Makala

Sina nyota ya mapenzi, sijapata mwanamke wa kuniambia ananitamani, Pasta Kanyari alalamika

April 14th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

PASTA mwenye utata Victor Kanyari, ambaye ni mwazilishi wa kanisa la Salvation and Healing Ministry amesema hana nyota ya mapenzi, miaka kadhaa baada ya aliyekuwa mkewe Betty Bayo kumuacha.

Pasta huyo aliambia Taifa Leo Dijitali kufikia sasa hajabahatika kutamaniwa na binti yeyote licha ya kuendeleza huduma ya uhubiri kwenye kanisa lake.

Alisema hata kanisani anapohubiri, hakuna mwanamke hata mmoja amewahi kujitokeza na kummezea mate.

“Sina bahati ya kupendwa na wanawake. Katika huduma ya uhubiri ambayo pia mimi husafiri sehemu mbalimbali hakuna wasichana ambao hunitamania, sijui sababu ni gani?” alifunguka Pasta Kanyari.

“Kufikia sasa umewahi kunipata kwenye skendo za wanawake? Skendo zangu zote huwa ni mambo ya pesa lakini sijawahi kuambiwa mambo ya wanawake,” aliongeza.

Baba huyo wa watoto wawili alifafanua kuwa likija suala la pesa, mara kwa mara jina lake huvutwa kwenye skendo hiyo. Alisema mapenzi ya pesa yamemfanya kukosa kuhusishwa kabisa na skendo za wanawake.

“Tuseme ukweli, nani hapendi pesa? Ukisema Kanyari anapenda pesa, wewe unachukia pesa?” aliuliza Bw Kanyari.

Licha ya kuachwa na msanii Betty Bayo, mhubiri huyo alikubali na hivyo hushiriki kwenye malezi ya wanawe wawili.

Pasta huyo alisema hutenga muda wa kuwa na wanawe.

“Nafurahia kukutana na wanangu na kula chakula pamoja nao,” alikamilisha Pasta Kanyari.

Mwaka jana, Pasta huyo alijiunga na mtandao wa TikTok. Amekuwa akitumia vipindi vya moja kwa moja na kupata zawadi kutoka kwa mashabiki. Zawadi hizo huwa ni malipo ya pesa.

Kwenye mahojiano ya mara kwa mara, husikika akiambia mashabiki “mnipatie zawadi, mimi ni mhubiri wa Mungu.”

Mchungaji huyo mara kwa mara husikika akiwaomba mashabiki wake wa TikTok kumtumia zawadi nyingi ikiwemo ile ya simba ambayo inatajwa kuwa yenye thamani kubwa (Sh40,000).

“Tuma zawadi, tuma zawadi. Nataka watu wajue mimi ni mtu wa Mungu. Tuma zawadi ya simba,” alisihi mashabiki wake.