Michezo

Sina tamaa ya hela, asema bondia Benson Gicharu baada ya kustaaafu

May 15th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HATIMAYE bondia Benson Gicharu ameangika glavu zake.

Afisa huyu wa polisi aliongeza kwamba hana mipango ya kujitosa katika ndondi za malipo jinsi wanamasumbwi wengi hufanya baada ya kuwakilisha mataifa yao.

“Nahisi wakati wangu wa kustaafu umewadia. Ni wakati mzuri mimi kupisha mabondia chipukizi ili pia waweze kuendeleza taaluma zao na kuwakilisha nchi,” alieleza Mei 14, 2018.

Gicharu, ambaye alizaliwa Mei 3 mwaka 1985, amekuwa katika taaluma hii kwa karibu miaka 20.

Katika kipindi hicho, amepeperusha bendera ya Kenya katika mashindano mbalimbali ya Bara Afrika, Jumuiya ya Madola na Olimpiki, miongoni mwa mengine.

Nyota yake ilianza kung’aa mwaka 2010 alipojishindia medali ya fedha katika michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Delhi nchini India. Alimlima Dexter Jordon kwa alama 8-0 katika robo-fainali ya uzani wa kilo 51 na kumlemea Oteng Oteng kutoka Botswana kwa alama 5-4 katika nusu-fainali kabla ya kupoteza dhidi ya Suranjoy Mayengbam kutoka India katika fainali.

Alivuna medali ya shaba katika uzani wa kilo 56 kwenye michezo ya Jumuiya Madola mjini Glasgow, Scotland mwaka 2014. Aliwazidi maarifa Sikiru Ojo (Nigeria) na Tafari Ebanks (Cayman) kwa alama 3-0 katika raundi ya 16-bora na robo-fainali, mtawalia, kabla ya kunyamazishwa na Muingereza Qais Ashfaq 3-0 katika nusu-fainali.

Gicharu alishiriki Olimpiki mwaka 2012 jijini London nchini Uingereza na 2016 jijini Rio de Janeiro nchini Brazil. Alibanduliwa nje katika hatua ya raundi ya 32-bora katika makala hayo mawili.