Michezo

Sina tamaa ya kuhamia Liverpool wala Man United – Wanyama

May 26th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Victor Wanyama amepuuzilia mbali kuondoka Tottenham Hotspur katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho licha ya ripoti kuenea anamezewa mate na Liverpool na Manchester United.

Nyota huyu mwenye umri wa miaka 26 alianza mechi nane pekee kati ya 38 za Ligi Kuu ya Uingereza msimu 2017-2018.

Wanyama alikuwa shabiki katika nusu ya kwanza ya msimu kutokana na jeraha baya la goti lililomweka mkekani miezi minne.

Licha ya kuandamwa na majeraha, vyombo vya habari nchini Uingereza vinasema Liverpool na Manchester United, ambazo ni klabu zinazojivunia mataji mengi ligini, 18 na 20, mtawalia, zinavutiwa sana naye na zinataka huduma zake.

Aidha, gazeti la Sun linadai kwamba kocha Mauricio Pochettino anaaminika kutafuta kuchangisha fedha kabla ya msimu 2018-2019 kuanza kwa kutema wachezaji kadhaa.

Akihojiwa na tovuti ya Goal, nahodha huyu wa timu ya taifa ya Kenya alisema, “Bado nina kandarasi na Spurs na lengo langu ni kuhakikisha naikamilisha.

“Sikuwa na msimu mzuri kutokana na jeraha na lengo langu sasa nikukazana wakati huu wa mapumziko kurejea kwa nguvu zaidi na kuisaidia kupata matokeo mazuri.”

Kandarasi ya Wanyama, ambaye mshahara wake ni Sh9.4 milioni kila wiki, itakamilika Juni 30 mwaka 2021. Alisajiliwa na Spurs Julai 1 mwaka 2016 kutoka Southampton.