Sindwele amtoroka dereva wake kutokana na ‘uchochole’

Sindwele amtoroka dereva wake kutokana na ‘uchochole’

Alifika shuleni Sidindi wakati mbaya. Alipouliza kama kampata Pengo, aliambiwa kuwa mwenzake huyu alikuwa kahudhuria warsha juu ya njia mbadala za kuendesha vipindi katika nyakati hizi ngumu za maenezi ya virusi vya corona.

Walimu na wafanyikazi waliokutika huko hawakuwa na muda naye. Walimpita kwenye eneo la mapokezi kana kwamba alikuwa sanamu.

Waliingia na kuondoka afisi hii na ile. Wengine walikuwa darasani wakijitahidi kuyaingiza maarifa kwenye vichwa vya wanafunzi. Wapo waliopita huku na kule. Shughuli tele almuradi kila mtu alishika hamsini zake.

Sindwele alitazama huku na kule asimwone yeyote aliyeguswa na uwepo wake pale. Mhazili alikuwa amemjibu kwa kauli moja tu, “Mwalimu Pengo hayuko, ameondoka kwa shughuli rasmi.”

Mhazili hakujisumbua kutaka kujua sababu ya ujio wa huyu mgeni. Alichosema tu ni kuwa Pengo hayuko. Hakusema zaidi, badala yake alijizika kwenye tarakilishi iliyokuwa mbele yake, kisha kama wenzake shuleni humu, akashika hamsini zake.

Sindwele hakuhitaji kuambiwa kuwa mazingira ya wachapakazi kama yale hayangemweka mzembe kama yeye.

Kukuru kakara za pale zilitosha kumwinua kitini na kumwondoa hapo kwenye makaribisho. Akajiondoa kuelekea nyumbani.

Alipiga hatua kuelekea kwenye lango kuu lakini akamkumbuka mdai wake aliyesubiri pale langoni. Angemlipa nini? Alikuwa katarajia kumwomba Pengo nauli, sasa Pengo mwenyewe hapatikani. Angejitetea vipi kwa mdai huyu?

Angesema lipi likasikiwa?Waendeshaji wa pikipiki waliamini kuwa walimu walikuwa na pesa nyingi. Alikumbuka mjadala wake siku moja na mwendeshaji wa pikipiki fulani.

Mwendeshaji huyo wa pikipiki aliamini kuwa walimu walilipwa mshahara mkubwa. Akasema kuwa hata siku za corona walimu waliendelea kulipwa. Aliongea kana kwamba walimu hawakupaswa kulipwa chochote.

‘Waendeshaji hawa wa pikipiki siwapendi. Wote wahuni utadhani walizaliwa na mama mmoja’ Sindwele alijiambia huku akielekea nje ya kiambo cha shule kwa kutumia lango la nyuma la shule hiyo.

‘Sitasumbuliwa na michuki kisha nisumbuliwe na vijana wadogo wa bodaboda! Huyo bwana mdogo akafanyie huko hayo macho yake makubwa kama njugu mawe.’

Sindwele alijiambia baada ya kutia guu lake nje ya shule.Aliyesemekana kuwa na macho makubwa kama njugu mawe alikuwa kwenye lango kuu akimsubiri mteja wake. Alimkatalia mbali kila mteja aliyeomba huduma za pikipiki yake.

“Ninamsubiri mteja huku ndani!” alisema kwa mikogo kana kwamba mteja aliyesubiriwa alikuwa na funguo za mbingu. Laiti angalijua

.Mwendeshaji huyu wa pikipiki alisubiri hadi akaanza kushuku kuwa alikuwa kapigwa mafamba. Akajitoma humo shuleni kumtafuta mteja wake.

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Wapi utekelezwaji wa Ripoti ya Blokcheni?

Bila kuzingatia muktadha, neno ‘hakika’ halipaswi...