Michezo

Sing'oki Igwe licha ya vichapo, asema Zapata

September 26th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

SASA ni wazi kwamba Mkufunzi wa AFC Leopards Rodolfo Zapata haendi popote baada ya uvumi kuenea kwamba angewatoroka mibabe hao wa soka hapa nchini kufuatia kushindwa kwao na Sofapaka katika mechi ya nusu fainali ya ngao ya Sportpesa Jumapili Agosti 28, 2018.

Kocha huyo kutoka Argentina amejitokeza mwenyewe na kuhakikishia mashabiki wa mabingwa hao mara 13 wa KPL kwamba yupo, tena sana huku lengo lake mpya ni kuhakikisha Ingwe inang’aa sana msimu ujao.

“Kwa hakika sijui uvumi uliotanda mitandaoni kuhusu kujiuzulu kwangu ulitoka wapi. Ni ukweli kwamba baada ya kichapo cha Sofapaka tulifadhaika sana na nikaandaa mkutano na wanadimba wangu.

Nilijivunia huduma zao ndipo nikawaeleza msimu wetu umekwisha ila nikawafichulia kwamba nitatumia mechi zilizosalia kutia mizani kila mchezaji kabla ya kutoa ripoti yenye mapendekezo kwa Baraza kuu la klabu(NEC) kuhusu mahitaji yetu kabla ya msimu ujao,” akafafanua Zapata katika kikao na wanahabari.

Vile vile kocha huyo aliwataka mashabiki wa Ingwe kuwa watulivu na wenye subira wanapokisuka upya kikosi cha majabali hao wakilenga kuyashinda mataji mengi msimu ujao wa 2018/19.

“Hakuna maajabu katika fani ya soka. Tuna wachezaji chipukizi kama like Owade, Mike Kibwage, Marvin Nabwire, Mburu, Marita, Oburu, Owiti, Saad Musa, Mavisi, Marcus, Senaji na wengine wazuri. Ni muda tu kisha AFC Leopards itarejelea hadhi yake ya zama zile. Kile kinachojengwa hakifai kuvurugwa,” akahitimisha mkufunzi huyo.

Wakati uo huo Meneja wa Ingwe Gilbert Selebwa amesema kwamba sasa wanalenga kumaliza ligi ya KPL katika nafasi ya tatu zikiwa zimesalia mechi tatu msimu huu wa 2017/18 ukamilike.

Ingwe kwa sasa wanashikilia nafasi hiyo kwa alama 51, moja mbele ya nambari nne Ulinzi Stars na nambari tano Sofapaka wote wakiwa na alama 50.