Michezo

SING'OKI: Nyota kudumu Chelsea baada ya kukubali mkataba mpya

July 25th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

WINGA Callum Hudson-Odoi wa Chelsea amekubali mkataba mpya wa miaka mitano kuendelea kuichezea klabu hiyo ya Stamford Bridge.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 18, anajiunga na wenzake Ruben Loftus-Cheek na Mason Mount ambao wamekubali mikataba ya kudumu kwa muda mrefu.

Hudson-Odoi ambaye mapema mwaka 2019 aliitwa kwa mara ya kwanza na Gareth Southgate kuchezea timu ya taifa ya Uingereza, alikuwa na mpango wa kuhamia Bayern Munich ya Bundesliga baada ya kupuuzwa na kocha Maurizo Sarri aliyeondoka majuzi.

Kiungo Callum Hudson-Odoi (kati) akiwa na madaktari baada ya kupata jeraha Aprili 22, 2019, Chelsea ilipoalika Burnley uwanjani Stamford Bridge, London. Picha/ AFP

Chelsea walikataa kufanya mazungumzo na Bayern mara tu nyota huyo alipoanza kupata nafasi katika kikosi cha kwanza, msimu ulipokuwa ukielekea ukingoni, kabla ya kuumia mguu Chelsea wakicheza na Burnley mnamo Aprili 23.

Bayern walikuwa wameweka mezani Sh5.2 bilioni kumtwaa staa huyo ambaye alicheza mechi 24 chini ya Sarri na kufunga mabao matano. Lakini Frank Lampard aliyesajiliwa kujaza nafasi ya Sarri anaonelea kinda huyo atakuwa muhimu kikosini baada ya Eden Hazard kuyoyomea Real Madrid, na sasa atakuwa akipokea Sh15 milioni kwa wiki

Lampard anamsubiri kinda huyo kwa hamu arejee kabla ya msimu mpya kuanza.

“Sitaki kusema mengi kumhusu, lakini talanta yake itakuwa muhimu kwa kikosi hiki pamoja na timu ya taifa kwa jumla,” alisema kiungo huyo mstaafu ambaye aliichezea Chelsea kwa zaidi ya miaka 10.

Kadhalika, Chelsea wanapanga kumuachilia Dujon Sterling ajiunge na Queens Park Rangers kwa mkopo, huku Jake Clarke-Salter akitarajiwa kujiunga na ama Birimingham City, Leeds United au Swansea City.

Fikayo Tomori aliyevuma chini ya Lampard katika klabu ya Derby City, huenda akajiunga na Chelsea.

Matt Miazga amerejea Reading huku Lewis Baker akijiunga na Fortuna Dussedorf

Hudson-Odoi anatarajiwa kurejea mazoezini mwezi ujao wa Agosti baada ya kukaa nje kwa miezi minne.

Kuelewa mfumo

Wakati huo huo, Lampard anaamini wachezaji wake wameelewa haraka mfumo wake kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya FC Barcelona katika mechi ya kirafiki nchini Japan.

Kocha huyo anayeshikilia rekodi ya Chelsea ya ufungaji mabao alisema juhudi za wachezaji wake mazoezini zinampa matumaini makubwa.

“Nimefurahia bidii ya kila mtu uwanjani,” Lampard alisema Jumanne akiwa Saitama, Kaskazini mwa Tokyo.

Akaongeza: “Kwa hakika, leo nimeona wachezaji wote wakifuata maagizo yangu, jambo ambalo ni la manufaa zaidi kwa kikosi kizima, na kwangu binafsi. Kuna mengi ya kufanya lakini imekuwa ziara nzuri.”

Chelsea walicheza pia kwa kiwango cha juu dhidi ya mabingwa wa Japan, Kawasaki Frontate.