Habari

Sintofahamu shule zikifunguliwa leo hii

October 12th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

SHULE za msingi na za sekondari nchini zinafunguliwa hii leo huku kukiwa na changamoto tele zinazotishia kutatiza hata zaidi shughuli za masomo.

Kuanzia kwa ukosefu wa madarasa, vyoo, miundomsingi duni na hali ngumu ya kiuchumi, ni kitendawili kigumu kinachozua hali ya sintofahamu kwa wanafunzi, walimu na wazazi kwa jumla.

Katika eneo la Baringo Kusini, hatima ya wanafunzi zaidi ya 4,000 kutoka shule 15 haijulikani baada ya madarasa yao kuzama majini baada ya Ziwa Baringo na Bogoria kuvunja kingo. Wazazi katika eneo hilo walisema kuwa kuna mengi ya kufanywa kabla ya shule kufunguliwa tena.

“Tunaomba wanaohusika kuchukua hatua haraka. Shule ya Sekondari ya Ziwa Baringo kwa mfano imehamishiwa katika sehemu ya juu lakini hakuna ujenzi wowote umeanzishwa licha ya shule kufunguliwa. Hatua ya dharura inapaswa kuchukuliwa. Watoto wetu hawana popote pa kuita shule,” alisema Bw John Cheboi, mkazi wa Kampi Samaki.

Walielezea wasiwasi pia kuhusu watoto wao wanaosomea katika shule za bweni huku vyumba vya mabweni, maabara na ukumbi wa maakuli, vikiwa vimeharibiwa na mafuriko.

Katika Kaunti ya Homa Bay, walimu wakuu katika shule za umma wanahofia kuwa wanafunzi katika taasisi zao huenda watalazimika kukaa nyumbani kwa muda zaidi au kuhamia katika shule zilizo tayari kurejelea masomo.

Shule nyingi zilizoathiriwa hazina miundomsingi muhimu ikiwemo vyoo na madarasa ya kutosha.

Madarasa saba katika Shule ya Msingi ya Rakwaro Kamwala, Rachuonyo Kaskazini, hayana paa baada ya kubomolewa na upepo mwezi uliopita.

Katika Shule ya Msingi ya Simbi katika eneo hilo vilevile, madarasa ambayo yangetumiwa na wanafunzi sasa ni makao kwa familia zilizofurushwa makwao baada ya Ziwa Victoria kufurika huku ikikabiliwa pia na tatizo la kukosa vyoo.

Shule nyingi za kibinafsi pia huenda zikakosa kufunguliwa baada ya kufungwa kwa miezi kadhaa huku wamiliki wakiitaka serikali kuwaongeza muda zaidi wa kufanyia miundomsingi ukarabati.

Shule hizo zinakabiliwa na changamoto ya kukosa walimu baada ya wengi wao kuhamia mashambani kutokana na nyakati ngumu za kiuchumi kuhusiana na Covid-19, ambapo watahitaji usadizi ili kuanza upya maisha mijini.

Wafanyabiashara walilalamikia uhaba wa wateja licha ya serikali kutangaza ufunguzi wa shule hii leo.

Matumaini yao kuhusu kuimarika kwa biashara zao kutokana na tangazo la shule kufunguliwa tena yalikatizwa huku wakistaajabu kuona wateja wachache tu wakijitokeza.

‘Bidhaa za shule bado zingalipo kwa sababu zilitumiwa muhula mmoja pekee. Wanaonunua ni wale ambao sare za watoto wao zimekuwa ndogo lakini wengi wananunua tu soksi,’ akasema.

Wazazi pia wamelalamikia kukosa uwezo wa kununua vifaa vya shule kutokana na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na athari za Covid-19 na kuishutumu serikali kwa kuwashitukiza tu kuhusu hatua ya ufunguzi wa shule.

Aidha, wazazi wameilaumu serikali kwa kuwakanganya kwa kutoa habari tofauti tofauti kuhusu tarehe ya kurejelewa masomo nchini.

‘Corona imeleta matatizo mengi nchini ikiwa ni pamoja na watu kufutwa kazi huku wengine wakipunguziwa mishahara. Hivyo basi, wengi wetu hatuna uwezo wa kununua bidhaa ambazo watoto wetu wanahitaji. Wamekuwa wakitupa habari za kutukanganya. Wengi wetu tulikuwa tumepanga kurudisha watoto wetu shuleni mwaka ujao. Pia hatuna uhakika iwapo watoto wetu watakuwa salama katika shule ikizingatiwa kuwa wanatoka maeneo mbalimbali,’ alisema Bi Saida

Abdallah, mkazi Mombasa.Ripoti Za Florah Koech, Mishi Gongo, George Odiwuor na Titus Ominde