Siasa

Siogopi kukabili Ruto debeni 2022 – Raila

December 25th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, amesema kuwa haogopi ushindani wa kisiasa kutoka kwa Naibu Rais William Ruto, ikiwa wawili hao watawania urais mwaka 2022.

Ingawa hajaweka wazi ikiwa atawania urais kwenye uchaguzi huo, Bw Odinga alimtaja Dkt Ruto kama “mtu mdogo” ambaye kamwe hawezi kumtisha kwenye ushindani wowote wa kisiasa.

Kwenye mahojiano mnamo Jumatano usiku, Bw Odinga alipuuzilia mbali kampeni za Hustler Nation (Watu Maskini) ambazo Dkt Ruto amekuwa akiziendesha, kama njia ya kuwapumbaza na kuwapotosha Wakenya.

“Wakenya ni watu werevu na wanafahamu kuwa kampeni hizo (Hustler Nation) ni za kuwapotosha. Wanajua kuhusu aina ya viongozi wanaowataka. Hivyo, simwogopi, kwani hilo ni wimbi linalopita,” akasema Bw Odinga.

Kauli yake inajiri wiki moja baada ya chama cha ODM kushindwa na mrengo wa Dkt Ruto kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni, Kaunti ya Kwale, ambalo chama hicho kilikuwa kikishikilia.Mwaniaji huru Feisal Bader aliibuka mshindi kwa kupata kura 15, 251 dhidi ya mwaniaji Omar Boga (ODM) aliyezoa kura 10,444.

Ikizingatiwa kuwa Bw Bader aliungwa mkono na Dkt Ruto, ushindi wake umezua msisimko wa kisiasa katika kundi la Tangatanga, baadhi ya wanachama wake wakidai ushindi huo ni ishara huenda Dkt Ruto akaibuka mshindi kwenye kivumbi cha urais 2022.

Dkt Ruto pia amekuwa akiendesha kampeni zake katika maeneo mbalimbali nchini, akishikilia kuwa nia yake ni “kuwainua watu maskini”.

Lakini mnamo Jumatano, Bw Odinga alimlaumu Dkt Ruto kwa kuendelea kutoa ahadi hewa kwa Wakenya, ilhali amekuwa serikalini kama naibu rais tangu 2013.

Alisema hapaswi kumlaumu Rais Uhuru Kenyatta kwa changamoto zinazowaathiri Wakenya, kwani amekuwepo wakati serikali imekuwa ikibuni mikakati inayotekelezwa.

“Dkt Ruto hawezi kujitenga na matatizo yanayowakumba Wakenya na kuanza kutoa ahadi mpya kwani amekuwa serikalini wakati mipango iliyopo inatekelezwa. Ni sawa na mimi kuanza kumlaumu Rais Mstaafu Mwai Kibaki kwa matatizo yaliyotokea wakati wa Serikali ya Muungano ilhali tulihudumu pamoja naye,” akasema.

Bw Odinga pia aliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuharakisha mchakato wa kukagua uhalali wa saini zilizowasilishwa kwake kuhusu ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), akisema haipaswi kutoa kisingizio chochote hasa baada ya kupokea fedha kutoka kwa Wizara ya Fedha.

Alisema kinyume na kauli ya IEBC kuwa huenda shughuli hiyo ikachukua zaidi ya mwezi mmoja, Bw Odinga alishikilia kuwa harakati hiyo haipaswi kuchukua zaidi ya wiki mbili. Tayari, IEBC imetangaza nafasi za makarani 400 kuisaidia kuendesha shughuli hiyo, baada ya kupokea Sh93.7 milioni.

“Ni kinaya kwa IEBC kusema itachukua muda kabla ya kumaliza harakati hiyo. Inashangaza kwani kundi lililokusanya saini hizo kutoka kwa Wakenya halikuhitaji makarani wowote kuthibitisha uhalali wake,” akasema.

Bw Odinga amekuwa akishinikiza tume hiyo kufanyiwa mageuzi, akisema imefeli kujenga imani miongoni mwa Wakenya, hasa kuhusu vile ambavyo imekuwa ikiendesha chaguzi kuu.