Habari MsetoSiasa

Siogopi kurudi debeni – Alfred Mutua

June 19th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

GAVANA wa Machakos Alfred Mutua amesema haogopi kurudi kwa debe endapo Mahakama ya Juu haitakubali ombi lake la kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa iliyofutilia mbali ushindi wake.

Ushindi wa gavana huyo ulifutiliwa mbali kufuatia malalamishi yaliyowasilishwa na mpinzani wake, Bi Wavinya Ndeti wa Chama cha Wiper.

Kulingana na Dkt Mutua (pichani), alikumbwa na pingamizi kali la upinzani kutoka kwa Muungano wa NASA wakati wa uchaguzi uliopita lakini akastahimili na kuibuka mshindi na hivyo basi anaamini anaweza kushinda tena kwa sababu umaarufu wa upinzani umepungua katika kaunti hiyo.

Alisema uamuzi wake kwenda Mahakama ya Juu ulitokana na kuwa anaamini alitumia njia za uadilifu katika uchaguzi uliopita.

Kiongozi huyo wa Chama cha Maendeleo Chap Chap alionekana kutiwa moyo na muafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambao umepunguza uhasama wa kisiasa kitaifa.

“Nilikuwa ninapingwa vikali kwa sababu ya kumuunga mkono Uhuru Kenyatta,” akasema kwenye mahojiano katika Runinga ya Citizen, Jumapili usiku.

Katika mahojiano hayo, Dkt Mutua alipuuzilia mbali wakosoaji wake ambao hudai anatumia muda mwingi kujienezea sifa katika vyombo vya habari ilhali hakuna maendeleo ya kweli aliyofanya mashinani.

Alisema kama ni kweli kuwa hajaleta maendeleo Machakos, hangeibuka mshindi kwenye uchaguzi wa mwaka uliopita.

Gavana huyo aliongeza kwamba ataorodhesha miradi yote ya maji aliyotekeleza na ataweka ramani ili wanaotilia shaka miradi hiyo waende wakajionee wenyewe.

Alirejelea matamshi yake kwamba ana orodha ya mawaziri, maseneta na viongozi wengine wakuu serikalini waliohusika kwa ufisadi na kutoa wito kwa Rais Kenyatta akabiliane vikali na wandani wake katika ikulu ambao wanashukiwa kuhusika katika ufisadi kwa vile anaamini rais pia ana orodha hiyo.

Aliongeza kuwa ufisadi upo pia katika serikali za kaunti akadai kuna magavana ambao hupokea hadi asilimia kumi ya malipo ya zabuni ambazo hutolewa kwa njia za ulaghai akaunga mkono hatua ya serikali kutaka maafisa wote wachunguzwe walivyopata mali zao.