Siraj: Nitasalia Harambee Stars

Siraj: Nitasalia Harambee Stars

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

BEKI mahiri wa Bandari FC, Siraj Mohamed amesema atapigania kuhakikisha anabakia katika kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Harambee Stars kitakachopambana na Uganda na Rwanda kwenye mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Siraj ambaye mashabiki wengi wa jimbo la Pwani wamekuwa wakilalamika kuachwa kwake katika timu hiyo ya taifa anasema atafanya bidii kwenye mazoezi ya kujitayarisha kwa mechi hizo ili apate namba katika kikosi cha kwanza.

“Nimekuwa na hamu ya kuchezea timu ya taifa, na kwa kuwa sasa nimechaguliwa, nitafanya bidii niwaridhishe maafisa wa benchi la ufundi kunibakisha kwenye kikosi kitakachokutana na timu pinzani,” akasema beki huyo.

Siraj aliwashukuru wachezaji wenzake, wakuu wa benchi ya kiufundi, viongozi wa klabu na mashabiki wa timu yake hiyo ya Bandari pamoja na wa jimbo la Pwani ambao wamekuwa na hamu kubwa na kumuombea kutaka achaguliwe kwenye kikosi cha Stars.

“Nawaahidi Wakenya kuwa sitawabwaga bali nitafanya bidii kuhakikisha ninapata namba katika kikosi cha kwanza. Nimekuwa na hamu ya kuvaa jezi ya nchi yangu, nimepata fursa hii na nitajitahidi kuitumikia kwa uwezo wangu wote,” akasema.

Kuhusu hali ya mchezo wake msimu huu, Siraj amesema haukuwa mbaya ingawaje janga la corona lilosababisha kusimamishwa kwa mechi kwa kipindi cha mwezi mmoja unusu liliathiri kidogo hali ya wachezaji wengi kwa sababu hawakuwa wakifanya mazoezi ya pamoja.

You can share this post!

Wakili ataka Jumwa amlipe Sh22.6m

Guardiola kuagana na Man-City 2023 akimezea ukocha wa timu...