Michezo

Siri ya Asante Kotoko kuizima Kariobangi Sharks yafichuliwa

December 20th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NAIBU wa timu ya taifa ya soka ya Ghana, Maxwell Konadu ameishauri Asante Kotoko iwe macho zaidi na washambuliaji wa Kariobangi Sharks klabu hizi zitakapomenyana katika mechi ya marudiano ya Kombe la Mashirikisho mjini Kumasi mnamo Desemba 22, 2018.

Tovuti ya Ghana Soccernet imesema Jumatano kwamba Konadu, ambaye aliongoza miamba hawa wa Ghana kushinda Ligi Kuu msimu 2011-2012, anapigia upatu Kotoko, lakini ameionya itakuwa na kibarua kigumu ikikubali kufungwa bao “kwa hivyo haifai kutumia mbinu itakayoalika mashambulizi” kutoka kwa mabingwa hao wa Kenya wa soka ya SportPesa Shield.

“Ile sare ya 0-0 iliyopatikana jijini Nairobi ilikuwa nzuri sana, lakini inaipa kila timu asilimia 50 ya kushinda, ambayo ni hatari.

“Najua (Sharks) wanakuja Ghana kujaribu kupata bao. Nimewachunguza na ninaona lengo lao ni kufunga bao na wala si kutumia mbinu ya kuzuia. Swali kubwa ni jinsi Kotoko itafanikiwa kuibuka na ushindi inapofanya mashambulizi na pia ikijichunga isiadhibiwe, kufanya kazi hiyo na kuifanya vyema,” tovuti hiyo imemnukuu akiambia redio ya Oyerepa FM.

“Hawatakuwa na pupa ya kufanya mashambulizi wakitangulia kufunga bao na hata Kotoko ikisawazisha, itakuwa 1-1. Kotoko inastahili kuwa macho kabisa, inastahili kupata mabao.”

Sharks na Kotoko zitakabiliana uwanjani Baba Yara kuanzia saa kumi na mbili na nusu jioni Jumamosi.

Sharks, ambayo inanolewa na William Muluya, iliingia raundi hii ya kwanza kwa kubandua nje Arta Solar7 ya Djibouti kwa jumla ya mabao 9-1. Kotko ilipata tiketi ya bwerere baada ya Cameroon kukosa kutaja mwakilishi wake kufikia siku ya mwisho ya kufanya hivyo hapo Oktoba 15, 2018. Mshindi kati ya Sharks na Kotoko ataingia raundi ya muondoano dhidi ya timu zitakazopoteza mechi za Klabu Bingwa Afrika katika raundi ya kwanza. Kisha, washindi watingia katika mechi za makundi. Droo za mechi za raundi ya muondoano na mechi za makundi zitafanywa Desemba 28, 2018 na Januari 21, 2019, mtawalia.