Habari Mseto

Siri ya Bondo iko karibu kuiva, Musalia aambia watu wa Siaya

February 5th, 2024 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MKUU wa mawaziri Musalia Mudavadi amesisitiza kuwa huenda Rais William Ruto ‘akakumbatiana’ na kinara wa upinzani Raila Odinga alivyoashiria wiki jana akiwa Bondo, Siaya, kaunti ya nyumbani ya waziri mkuu huyo wa zamani.

Akizungumza akiwa Kakamega jana, Bw Mudavadi alisisitiza kuwa alitumwa na Rais Ruto kumwakilisha Bondo na kwamba kuna mambo mazuri njiani yatakayowafurahisha wakazi wa eneo hilo.

Aliwataka wakazi wa eneo la Magharibi kuendelea kuunga serikali ili nao wafurahie mazuri. Aliwaambia wafuasi wa Kenya Kwanza wasishangae iwapo hali ya kisiasa itabadilika Bondo.

“Wiki iliyopita nilikuwa China kukutana na mwenzangu wa Mashauri ya Kigeni. Mara tu baada ya kutua Kenya, nilipewa kazi maalum Bondo,” alieleza.

Zaidi ya hayo, Bw Musalia alisema kama si majukumu ya kimataifa, Rais angeenda Bondo, safari aliyosema ingeleta mabadiliko ya kisiasa.

“Rais alikuwa anaelekea Italia na alinipa jukumu la kumwakilisha Bondo. Niliwaambia wenyeji wa Bondo kukumbatia serikali ya Ruto kwani hawajui kitakachotokea,” akaeleza.

Akiwa Bondo mnamo Januari 28, Musalia aliwaambia wakazi wa eneo hilo kutarajia kupokea habari njema.

“Nakili tarehe hii na mahali ambapo nimesema hivi,” Musalia alisema wakati huo.

Jumapili alirudia hayo mbele ya Rais Ruto.