Siri ya kufanikisha ufugaji wa kuku hii hapa

Siri ya kufanikisha ufugaji wa kuku hii hapa

Na SAMMY WAWERU

MITA chache kutoka mtaa wa Mumbi, Ruiru, Kaunti ya Kiambu ndiko Mzee Henry Njoroge huendeleza ufugaji wa kuku.

Katika mandhari tulivu, kinachokukaribisha katika boma lake ni koo (kuku jike) na jogoo wanaozunguka kujitafutia lishe.

Mzee Njoroge ni mfugaji wa kuku halisi wa kienyeji. “Huwafuga kwa minajili ya mayai,” asema.

Huwageuza kuwa wa nyama, japo wachache, haja inapoibuka hususan msimu wa Krismasi au anapopata wageni.

Ni ufugaji-biashara ambao hajauanza leo, jana wala juzi.

Umri wake ukionekana kusonga, yaani kula chumvi ni ufugaji anaouendeleza kama kijana barobaro.

Anafichua, katika kila chumba cha boma lake hakikosi kuku anayeatamia (kulalia mayai) na aliyeangua vifaranga.

Isitoshe, kuna wanaotaga mayai akisema wengine hutagia katika vichaka vidogo vya ploti yake.

“Kibarua huwa kukusanya mayai hasa kwa wasiotagia kwenye vizimba vidogo katika nyumba,” aelezea.

Hata ingawa hana takwimu za idadi jumla ya kuku alionao, Njoroge anasema kwa wiki hakosi kufanya mauzo ya mayai.

Kaunti ya Kiambu na Nairobi, trei ya mayai halisi ya kienyeji haipungui Sh600.

Trei ina idadi jumla ya mayai 30, na hii ina maana kuwa yai ni Sh20.

Wakati wa mahojiano na Akilimali, tulimpata akiwa na kuku kadhaa walioandamana na vifaranga, kila mmoja akiwa na wana wasiopungua 10.

“Huangua kadri ya vifaranga 10 – 15,” akaelezea, akionekana kuridhishwa na ufugaji aliokumbatia.

Mzee Henry Njoroge ni mfugaji wa kuku halisi wa kienyeji eneo la Mumbi, Ruiru, Kaunti ya Kiambu. PICHA | SAMMY WAWERU

Kulingana na mfugaji huyu ambaye ni mcha Mungu, kinachochangia kufanikisha jitihada zake ni bidii.

Anasema kufuatia uzoefu wa miaka mingi katika ufugaji, amegundua ili kuku awe na mazao ya kuridhisha anapaswa kutunzwa vyema baada ya kifaranga kuanguliwa.

Maradhi yanayotajwa kuhangaisha kuku ni; Fowl Cholera, Coccidiosis, Avian Influenza, Fowl Pox, Newcastle, na Salmonellosis.

Mfugaji huyu anasema siri kuyaepuka ni kuchanja vifaranga wanapoanguliwa, pamoja na kuzingatia ushauri wa mavetinari kitaalamu.

“Vifaranga wangu wanapoanguliwa, huwachanja na kuwapa dawa kama vile Liquid paraffin kati ya nyinginezo kwa mujibu wa mapendekezo ya vetinari,” afichua.

Aidha, liquid paraffin huwatilia kwenye vifaa vya maji. “Wakinywa juma moja au mawili, kinga yao itakuwa imara”.

Ni hatua anazosisitiza huwaondolea ndege wake hao wa nyumbani kero ya magonjwa.

“Wafugaji wengi hufeli kwa sababu ya kutochanja vifaranga hasa wanapoanguliwa.

“Ni muhimu wazingatie taratibu faafu kitaalamu kufanikisha ufugaji kuku. Sawa na mtoto anapozaliwa hupata chanjo kadhaa, za kuku pia zipo,” afafanua Simon Wagura, mtaalamu.

Muhimu zaidi, kulingana na mtaalamu mwingine, James Muthua ni kuzingatia kiwango cha usafi.

“Vizimba, vifaa vya kuwatilia malisho na maji na mazingira ya ndege kwa jumla yawe safi ili kukwepa kero ya maradhi ya ndege na ndege na yale ibuk,” Muthua ashauri.

Katika boma la Mzee Njoroge, kwenye ua yake amekuza mmea asilia aina ya aloe vera au mshubiri na pilipili hoho, mimea anayotumia kukinga kuku dhidi ya magonjwa ibuka.

“Matibabu ya kienyeji pia yanasaidia kulinda kuku,” asema.

Huku gharama ya chakula ch madukani cha mifugo ikitishia wafugaji kutokana na mfumko wa bei, Njoroge anaipunguza kwa kuwapa punje za mahindi.

Husaga mahindi, ambapo huyatia madini ili kuongeza virutubisho faafu.

Vilevile, huwapa mboga, ambapo hukuza sukuma wiki, spinachi na zile za kienyeji katika mazingira yake.

Isitoshe, kuku wake hujisakia lishe hasa wanapofunguliwa kupunga hewa safi na mwanana.

Yote tisa, kumi huhakikisha kuku wake wanapata maji safi na ya kutosha. Aidha, Mzee Njoroge ana mfanyakazi mmoja.

You can share this post!

Nigeria yaondolea Twitter marufuku

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Wakati ni amana na rasilimali kubwa...

T L