Akili Mali

Siri ya kufaulu katika ufugaji ng’ombe wa maziwa


KATIKA Wadi ya Kakrao, Suna Mashariki, Kaunti ya Migori, Paul Odeny, 27, anatumia shamba lake la ekari 10 kwa kilimo mseto.

Mtindo huu umemfanya kuwa kielelezo cha uvumbuzi na uendelevu wa kilimo.

Mkurugenzi huyu wa Kaks Farms, anajikita katika ufugaji wa ng’ombe aina za Friesians, Ayrshire na Sahiwal.

Yeye hutekeleza mikakati ya kuhakikisha uzalishaji wa maziwa bora na udumishaji maslahi ya mifugo.

Ukuzaji malisho

Huku akikabiliwa na gharama kubwa za malisho, Bw Odeny hukuza lishe yake mwenyewe. Malisho haya hujumuisha mahindi, brachiaria, majani ya viazi vitamu, calliandra, nyasi ya napier na maharagwe.

Kujitosheleza huku kunapunguza gharama na kumpa udhibiti wa ubora wa malisho. “Mkulima makini lazima awe na udhibiti wa uzalishaji wake wa chakula,” anasema.

“Mbinu hii haipunguzi tu gharama lakini pia inahakikisha lishe ina thamani ambayo ni muhimu kwa kudumisha afya ya mifugo.”

Bw Odeny hutumia mfumo wa Total Mixed Ration (TMR) ambao huchanganya viungo vyote vya malisho katika mchanganyiko mmoja.

“Husaidia kuwekeza na kukumbatia lishe bora ambayo si tu ya bei nafuu bali pia inachangia uzalishaji mkubwa wa maziwa,” aeleza.

Utaratibu wa Kulisha

Paul Odeny akitengeneza chakula cha mifugo kwa ajili ya ng’ombe wake. PICHA | LABAAN SHABAAN

Bw Odeny na wafanyakazi huanza kukamua saa kumi na moja asubuhi na kurejelea shughuli hiyo saa hizo hizo jioni.

Kila ng’ombe wake 31 hutoa angalau lita 20 za maziwa kwa siku. Mchakato huu wa ukamuaji huanza kwa usafi wa kiwele cha ng’ombe.

“Mimi huhakikisha ng’ombe wangu wanapata matunzo na uangalizi wanaohitaji ili kuzalisha maziwa mengi,” Bw Odeny anaeleza.

Kila siku saa moja asubuhi, ng’ombe hawa hupokea chakula cha TMR ambacho ni mseto wa nyasi, nafaka, silaji ya mahindi, protini, vitamini na madini.

Taratibu za Kilimo Endelevu

Usindikaji wa malisho katika shamba la Kaks, Suna Mashariki, Kaunti ya Migori. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Wasipokuwa katika shughuli za kula, kulala au kukamuliwa, wao hushughulika kutengeneza samadi ambayo ni muhimu katika ukuzaji wa malisho yao,” Bw Odeny anabainisha.

Uendelevu ni msingi wa harakati za kilimo katika shamba la Bw Odeny. Kwa kukuza lishe yake mwenyewe, yeye hupunguza utegemezi wa malisho ya dukani.

Mbolea itokayo kwa wanyama wake pia husaidia kupunguza gharama ya kilimo.

“Tumeajiri wakulima wanne ambao tumewatwika jukumu muhimu la kudumisha shughuli za shamba,” anaeleza.

Mikakati ya Soko

Maziwa yanayozalishwa na Bw Odeny hufikia wateja mbalimbali na masoko.

Wateja hawa hujumuisha wasindikaji wa maziwa, wanunuzi wa jumla na mauzo ya moja kwa moja kwa watumiaji.

“Mara nyingi mimi huuza moja kwa moja kwa wateja kupitia mauzo ya shambani. Hii inaniruhusu kuanzisha uhusiano wa karibu na watumiaji ili kupata faida kubwa ikilinganishwa na kuuza kupitia mabroka,” anafichua.