Pambo

Siri ya kuwa na furaha maishani

March 24th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KATIKA nyakati hizi ambapo Wakenya wengi wanapitia hali ngumu kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, aliyekuwa gavana wa Meru Kiraitu Murungi amebuni ‘tiba’ kwa mahangaiko wanayopitia watu wengi.

Bw Murungi anasisitiza kuwa lazima Wakenya waanze kukumbatia furaha na kicheko kama njia ya kufuta mahangaiko hayo.

Huo ndio ujumbe mkuu ambao kiongozi huyo alitoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Furaha mnamo Jumatano.

Siku hiyo ilirasimishwa na Umoja wa Mataifa (UN) mnamo 2012 na hudhimishwa kila Machi 20.

Sherehe za kuiadhimisha siku hiyo hapa nchini zilinoga sana jijini Nairobi.

Katika kile kilionekana kama mwanzo rasmi wa sherehe hizo nchini, Bw Murungi aliongoza shughuli za uzinduzi wa Furaha Kenya Club.

“Wakati umefika tuanze kukita maisha yetu katika masuala ya furaha, upendo na kicheko. Tunaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Furaha ili kujikumbusha kuhusu furaha na umuhimu wa furaha katika maisha yetu; na muhimu zaidi, duniani kote,” akasema Bw Murungi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Sheria (KSL), Prof Patrick Lumumba, alisema kuwa licha ya changamoto nyingi ambazo Wakenya wanapitia, wanafaa kutafuta na kubuni njia za kupata furaha.

Alitoa wito kwa Wakenya na Afrika nzima kwa jumla kukumbatia uadhimishaji wa Siku ya Kimataifa ya Furaha, akisema watapata maana halisi ya kuishi.

“Si wengi wanaojua kwamba mnamo Juni 28, 2012, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lilipitisha Machi 20 kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Furaha. Inasikitisha kuwa siku hii haisherehekewi kwa mbwembwe zinazofaa,” akasema.

Kuzinduliwa kwa klabu hicho kunajiri baada ya Bw Murungi kusema mwaka uliopita kwamba, alikuwa ashakamilisha shahada ya digrii kutoka kwa Taasisi ya Mafunzo ya Furaha na kufuzu.

“Nina furaha kutangaza kwamba nimemaliza shahada ya digrii ya mwaka mmoja ya mafunzo ya furaha kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Furaha na kufuzu. Kwa sasa, nina ujuzi wa kutosha kuendesha mwamko mpya wa furaha katika nchi yangu,” akasema mnamo Novemba 2023.

Mwanasiasa huyo pia aliweka picha akiwa na watu wengine waliofuzu. Vile vile, aliweka picha ya cheti chake, ambapo kilikuwa kimetiwa saini na mwanzilishi wa taasisi hiyo, Dkt Tal Ben-Shahar.

Hatua ya Bw Murungi kujitosa katika masuala ya kueneza furaha ilitokana na kauli yake kuwa nusura ajipate kwenye mzongo wa kimawazo, baada ya kushindwa na Gavana Kawira Mwangaza wa Meru kwenye kinyang’anyiro cha ugavana katika uchaguzi wa 2022.