Dondoo

Siri ya mke wa nyumba mbili yafichuka

September 10th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

MWIKI, NAIROBI

Kalameni mmoja mtaani hapa, alipigwa na butwaa alipogundua kuwa mwanadada aliyeita mkewe alikuwa amekodi nyumba kwingine.

Inasemekana polo alipata habari hizi alipokuwa ameenda kumuona kipusa hospitalini baada ya kuugua.

Kulingana na mdokezi, polo alipofika hospitalini alikutana na marafiki wa mkewe waliokuwa wamemtembelea.

Inasemekana polo aliwarai wamtembelee rafiki yao nyumbani akitoka hospitalini.

“Sisi humtembelea kwake. Hata jana tulikuwa kwake tukaosha vyombo na kupiga deki,” rafiki mmoja wa kipusa alisema.

Polo alishindwa kuelewa ni nyumba gani waliyokuwa wakizungumzia kwa sababu hakuwa amewaona kwake.

“Kwani mlikuwa nyumbani saa ngapi?” polo aliuliza huku kipusa akijaribu kukatiza mazungumzo hayo.

Warembo waliendelea kumwaga maneno bila kujua wako mtegoni. Walitoa maelezo kikamilifu kuhusiana na nyumba ambayo kipusa alikuwa amekodi eneo fulani.

“Nyumba hiyo ni nani huwa analipa kodi?” polo aliuliza kiujanja.

Duru zinasema ilimbidi kipusa kukatiza mazungumzo hayo kwa hasira.

Penyenye zinasema hapo awali polo alikuwa ameshuku kuwa kipusa alikuwa na uhusiano wa kisiri na wanaume wengine.

“Mbona hii nyumba umekodi mimi siijui?” polo alimuuliza kipusa.

Inadaiwa kipusa hakuwa na jibu la kumpa mumewe. Warembo waliotoa habari hizi walibaki midomo wazi wasijue la kufanya.

Kulingana na mdokezi, kipusa alikuwa amewaeleza marafiki wake wote kuwa hajaolewa na huishi peke yake licha ya kuishi na polo kwa zaidi ya miaka mitano.

“Kila wakati huwa unapotea kwangu. Kumbe huwa unakutana na hawa watu kwa nyumba nyingine,” polo alijaribu kuongea huku hasira ikimpanda.

Mdokezi alieleza kuwa jamaa aliondoka kwa hasira baada ya kubaini mwanadada alikuwa akimcheza shere.