Makala

SIRI YA UFANISI: Hakunufaika na mpango wa unyunyiziaji maji, akajipanga

January 23rd, 2020 2 min read

Na SAMMY LUTTA

KIJIJI cha Katilu kilichoko kilomita chache kutoka barabara kuu ya Kitale-Lokichar kinatambulika sana kwa ukulima wa mimea tofauti tangu Bodi ya Kitaifa ya Unyunyuziaji maji (NIB) ilipoanzisha miradi yake eneo hilo 1970.

Kabla ya miradi hiyo, kijiji hicho kilikuwa miongoni mwa vijiji vingine katika Kaunti ndogo hiyo ya Turkana Kusini vilivyokuwa vikishuhudia uvamizi kutoka kwa wezi wa mifugo kutoka jamii jirani ya Pokot.

Ukulima ulikuwa njia mojawapo ya kuhakikisha Waturkana walioko kwenye mpaka wa jamii hizo mbili ambao walipoteza mifugo wao wanajifunza ukulima badala ya kuhama ama kutegemea chakula cha msaada.

Hata hivyo, Samuel Eiton, 28, ambaye tunampata kwenye shamba lake la ukubwa wa ekari mbili anasema kuwa japo shamba lake liko na miti 2,500 ya nyanya na mimea mingine kama sukuma wiki, spinachi, kabeji na vitunguu, kilichomfanya aanze ukulima, ni kukosa kila mara kwenye orodha ya wanaolengwa na NIB.

“Kutopata nafasi kama wakazi wengine ili kunufaika na mradi wa kunyunyuzia mashamba maji bila kuhitajika kutoa pesa zozote, ilikuwa kama baraka iliyojificha kwa sababu ilifanya nikawa na bidii na sasa naeza kupata mazao ya Sh520,000 kutoka kwa ekari zangu mbili,” Eiton alisema.

Miaka sita iliyopita, aliacha kufuga mbuzi kwa wingi kwa sababu walikuwa wakiibiwa na wezi wa mifugo alipokuwa akiachia watu wamchungue anapokuwa kwa kazi yake ya udereva.

Changamoto ya kwanza aliyopambana nayo ni kung’oa miti ya mathenge ambayo kando na kuwa na miba, mizizi yake ni mirefu sana.

Alitengeneza ekari moja ambayo alipanda mahindi kwa miaka miwili kabla ya afisa mmoja wa kilimo kumshauri apande mimea yenye faida nyingi na ambayo kwa kipande kidogo cha shamba atakuwa na mapato mengi kwa miezi michache.

“Kupitia kwa akiba ya fedha kutoka kwa mahindi, udereva na kuuza mbuzi kadhaa nilianza kupanda nyanya na sukuma na kuacha mahindi,” Eiton mwenye watoto wanne alisema.

Alisema wanunuzi kutoka kijiji hicho na mji wa Lokichar walikuwa wengi na hata ikamlazimu kuajiri watu wanne wa kumsaidia kuongeza shamba kuwa ekari mbili.

“Niliekeza Sh200,000 kuanzisha ukulima. Nikanunua bomba za kutoa maji kutoka Mto Turkwel za Sh90, 000 ili mimea isikose maji.

Kando na miti 2,500 ya nyanya ya mbegu aina ya F1, nilipanda kabeji 600 ambazo baada ya kukomaa moja inauzwa Sh20,” alisema.

Anaeleza kuwa maeneo ya mpakani si mazuri kwa kufuga mbuzi kwa sababu wezi huiba sana eneo hilo.

Alieleza kuwa ni rahisi kushughulikia mimea kwa sababu si wengi wanajua ukulima.

Eiton alisema ndipo ufuge mbuzi wengi, ni lazima mtu ajihami kwa bunduki haramu na hiyo hairuhusiwi kisheria.

“Siwezi kuacha ukulima kwa sababu mpango wangu sasa ni baada ya mavuno yote natarajia kuongeza miti ya nyanya iwe 4,000 kwa sababu nilipata wateja wanaopenda nyanya zangu sokoni na hoteli kadhaa mjini Lodwar,” alisema.

Huku wakazi waliopoteza mifugo wakiwa na ulazima wa kupata mafunzo na uwezo wa kifedha ili kutengeneza shamba na kupanda mimea, Eiton anashauri mashirika hayo kuchagua maeneo ambayo hayajawai kupandwa mimea ili wenyewe watoe miti sugu ya mathenge.

“Wanaopata ufadhili wa ukulima ni vizuri pia watie bidii ili iwapo shirika lijiondoe baada ya miaka michache, isiwe mwisho wa mradi,” ashauri Eiton.

NIB kwa sasa ina shamba la ekari 2000 ambapo mimea kama mahindi, ndizi, mchele, dengu, mtama na tikiti maji hupandwa ili kufaidi wakulima 35,000.