Siri ya Young Elephant kutetemesha ligi

Siri ya Young Elephant kutetemesha ligi

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Young Elephant imeibuka moto wa kuotea mbali kwenye mechi za kuwania Ligi ya KYSD kwa wasiozidi umri wa miaka 12 muhula huu.

Kikosi hicho ambacho hutiwa makali na kocha, Jackson Amas kinazidi kutetemesha washiriki wengine baada ya kushiriki jumla ya mechi 15 bila kushindwa.

Kufikia sasa Y.Elephant imeshinda mechi 14 na kutoka nguvu sawa mara moja. Ufanisi huo umezitia hofu timu zingine ikiwamo mabingwa watetezi, Kinyago United iliokuwa ikiwinda kushinda taji hilo kwa mara ya 14.

”Kusema ukweli kwa jinsi tunavyoendelea hatuna la ziada tunataka kuendeleza mtindo wa kutembeza vipigo dhidi ya wapinzani wetu nia yetu ikiwa kuibuka mabingwa wa taji la msimu huu,” kocha huyo alisema na kuongeza kwamba kufikia sasa hawajaona sababu ya kutobeba taji hilo.

Kocha huyo bado anasisitiza kuwa chipukizi wake wamekaa vizuri kupambana mwanzo mwisho na wapinzani wao. Anadokeza kuwa ufanisi huo umewapa wachezaji wake motisha zaidi ambapo wameapa hawana lingine bali wamepania kushinda taji hilo ambalo wameliwinda kwa misimu mitano iliyopita.

Ingawa kikosi hicho kingali kileleni mwa jedwali kwenye kampeni hizo, kocha huyo anashikilia kuwa bado kunazo vikosi vinavyoweza kuzima matumaini yao kubeba taji hilo. Anataja baadhi ya wapinzani hao kama Young Lions, Fearl FC, Kinyago United. MASA FC na Blue Bentos kati ya zingine.

Chipukizi hao wanajivunia kushinda taji la Centre Eastleigh walipolaza Pro Legends FC katika fainali. Pia waliibuka mabingwa kwenye mashindano ya Shauri Moyo Youth, Pastor Jeremiah Tournament pia Vijana na Talanta. Kadhalika chipukizi hao wameshiriki mashindano mengine kama:Peace Tournament, Malezi Tournament, Pumwani Group Red Cross Tournament, KYSD Laegue na St Johns League.

Kikosi hicho kinajumuisha wachezaji kama Peter Morgan, John Aron, Musa Mutuma, Duncan Njoroge, Dickson Songola, Tobias Ochola, Khalid Musa, Duncan Onguong kati ya wengine. Kocha huyo husaidiana na naibu wake Issa Juma. Kipute cha KYSD muhula huu kinashirikisha jumla ya timu 18 ambazo sita kati yazo zinashiriki kwa mara ya kwanza.

Kwenye msimamo wa kipute hicho, Y.Elephat inaongoza kwa kuvuna alama 43, 12 mbele ya Young Lions. Kocha huyo anasema kuwa mechi za kipute cha KYSD zimeibuka msaada mkubwa kwa wachezaji chipukizi katika Kaunti ya Nairobi. Kituo cha Kinyago kinajivunia kukuza wachezaji wengi ambao baadaye wamefaulu kupata nafasi kuchezea klabu zinazoshiriki ligi za haiba ya juu nchini.

You can share this post!

NEOLIN MOMANYI: Hongera NMG kwa kujitolea kuangazia masuala...

Blue Boys yatwaa ushindi wa KYSD