Michezo

Sirudi ‘Misri’, asema Coutinho kuhusu Liverpool

February 15th, 2020 1 min read

GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

NYOTA Philippe Coutinho amepuuzilia mbali atajiunga tena na Liverpool mwisho wa msimu huu.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil yuko Bayern Munich kwa mkopo kutoka kwa Barcelona baada ya kusikitisha uwanjani Camp Nou.

Coutinho alitua Barcelona kutoka Liverpool kwa Sh18.6 bilioni katika kipindi kifupi cha uhamisho Januari 2018 baada ya miezi kadha ya fununu kuwa yumo mbioni kuelekea Camp Nou.

Kiungo huyo amehusishwa sana na kurejea uwanjani Anfield baada ya kukosa kuridhisha akivalia jezi ya mabingwa hao wa Uhispania. Hata hivyo, Coutinho amepuuzilia mbali uwezekano wake wa kuwa mchezaji wa Liverpool tena.

“Nilitoka huko na sina mpango wa kurudi huko. Nilichukua njia tofauti, na sasa niko katika safari yangu, kama tu kila mtu,” Coutinho amenukuliwa na gazeti la Sports Illustrated.

“Akili yangu yote iko katika kutimiza ndoto yangu. Nafurahia nilichofanyia klabu hiyo nilipokuwa mchezaji wake, na sasa mimi nalenga mbele.”

Coutinho hakuwa tegemeo Camp Nou ilivyotarajiwa akitokea Liverpool.

Alifungia Barca mabao 21 katika mechi 76 katika mashindano yote.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 ameanza kupata makali yake uwanjani Allianz Arena katika miezi chache amekuwa huko, akitikisa nyavu mara saba katika mechi 27.