HabariHabari Mseto

Sishuki hapa bila chai, mahabusu awahangaisha askari

February 20th, 2018 1 min read

Na GERALD BWISA

KULIZUKA kizaazaa katika mahakama ya Kitale  Jumanne asubuhi baada ya mmoja wa mahabusu kukataa kushuka kutoka kwa lori la gereza ili ahudhurie kikao cha kesi yake, akitaka kwanza apewe chai.

Mambo yalikuwa shwari lori hilo lililokuwa limejaa mahabusu wengine lilipoegeshwa katika uga wa mahakama, na kila mmoja akaanza kushuka kuingia kortini.

Hata hivyo, ilipowadia zamu ya mfungwa huyo aliye rumande, aliyetambulika tu kama Stephen, alipanda juu ya lori na kuanza kupiga kelele akitaka apewe chai kwanza.

Mwanamume huyu anayejulikana kwa jina moja Stephen, aliamua kuwahangaisha polisi Februari 20, 2018 alipokataa kushuka kutoka kwa lori lililowaleta washukiwa waliosukumwa rumande. Alisisitiza kuwa iwapo polisi walitaka ashuke, basi walifaa kumpa chai moto anywe kwanza ili apate nguvu za kutembea. Picha/ Gerald Bwisa

“Mimi sitoki hapa hadi nipewe chai,” akasema kwa nguvu.

Askari wa magereza waliosafiri na mahabusu hao ili kutoa ulinzi walipigwa na butwaa kabla kujikusanya na kuafikiana kumtuma mmoja wao akamshushe chini mtu huyo kwa lazima.

Maji yalizidi unga pale Stephen alimpiga chenga akiruka kutoka upande mmoja hadi mwingine kumkwepa askari huyo.

Baada ya mchezo wa paka na panya, hatimaye alinyakwa na kupelekwa moja kwa moja hadi kortini bila hata tone la chai. Picha/ Gerald Bwisa

Lakini ujanja wake ulifika kikomo aliponaswa na kuteremshwa chini.

Aidha, hakupewa hata tone ya chai huku akisindikizwa haraka upesi hadi seli na kupewa onyo kali akithubutu kurudia tena utundu huo.

Stephen anakabiliwa na shtaka la kuiba mahindi eneo la Cherangany. Alikuwa amefikishwa kortini pamoja na washtakiwa wengine ili kusikizwa kwa kesi hiyo.