Habari Mseto

Sita wafariki baada ya mashua kuzama

October 11th, 2020 2 min read

Na VICTOR RABALLA

WATU sita walifariki Ijumaa usiku wakati mashua waliyokuwa wakisafiria ilizama ndani ya Ziwa Victoria.

Mkasa huo ulitokea saa nne usiku eneo la Budalang’i, Kaunti ya Busia. Polisi walisema kwamba mashua hiyo ilikuwa imebeba watu 13 kutoka nchi jirani ya Uganda ilipozama.

Kulingana na mwenyekiti wa ufuo wa Sisenye, Bw Stephen Musee, mashua hiyo iliyotoka kisiwa cha Sigulu kilichoko Uganda ilikuwa ikielekea kutua ufuoni Sisenye upande wa Kenya.

“Kuna watu saba walionusurika na walipatikana alfajiri na wavuvi waliokuwa wakitoka kuvua samaki usiku ziwani,” alisema.

Manusura hao walikimbizwa hospitali ya kaunti ndogo ya Port Victoria ambapo wanaendelea kupata nafuu huku kikosi cha kudumisha usalama sehemu za pwani (Kenya Coast Guard) kikianza kusaka miili ya waliokufa.

“Tumetuma boti nne na wapiga mbizi kusaidia katika operesheni hiyo na tunatumai kuwa wataikamilisha haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Musee.

Alisema kuna raia watatu wa Uganda na Mkenya mmoja ambao hawajulikani waliko.

Alitaja majina yao kama Bridget Erumbi, Carol Odongo, Sebastián Akuku, Lucy Odimbo, David Muluka na Evans Okumu ambaye ni mmiliki wa mashua hiyo.

Bi Wilkister Ajiambo aliyepoteza mumewe, Sébastian Akuku, alisema alimuona mara ya mwisho Agosti.

“Alienda Uganda kulima nyanya baada ya mimea yake kusombwa na mafuriko ya hivi majuzi na alikuwa akileta mavuno ya kwanza mkasa ulipotokea,” alisema.

“Kulingana na mila zetu, nitapiga kambi hapa mpaka nitakapoona mwili wa mume wangu. Ninaomba mashirika ya serikali kutoa mashua za kusaidia kutafuta miili ili kutuondolea msononeko,” alisema Ajiambo ambaye ni mama ya watoto saba.

Jamaa wengine wa waliopoteza wapendwa wao pia waliomba serikali isaidie kutafuta mili ili waanze mipango ya mazishi.

Kamishna wa Kaunti ya Busia Joseph Kanyiri hata hivyo alisema waokoaji watatoa ripoti ya mwisho baada ya shughuli hiyo kukamilika.

Mkuu wa polisi eneo la Bunyala Jeferson Nyakundi alisema miongoni mwa waliokufa ni watoto wawili, mwanamke mmoja na nahodha wa mashua hiyo.

Aliwataka mabaharia kuwa makini kwa sababu mawimbi yanaweza kusababisha hasara akisema ni muhimu kuvalia jaketi za kuzuia kuzama.

Mkasa huo ulitokea miezi mitano baada ya mashua nyingine iliyokuwa na abiria 20 kuzama katika ufuo wa Usenge Kaunti ya Siaya.

Mbunge wa Budalang’i Bw Raphael Wanjala jana aliwaomboleza walioangamia na kufariji familia zao. Aliahidi kusaidia familia hizo wakati huu mgumu wa majonzi.