Michezo

Sita wajiondoa kwenye uchaguzi wa FKF

September 10th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

SIKU tisa kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wapya wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) katika kiwango cha kaunti, baadhi ya wawaniaji wa viti mbalimbali wamejiondoa katika kinyang’anyiro.

Wagombezi hao wanadai kwamba hawana imani na mchakato wa kufanikisha uchaguzi huo na dalili zote zinaashiria kuwa hapatakuwepo na haki na usawa hadi malalamiko yao kusikilizwa na Jopo la Mizozo ya Spoti (SDT).

Wawaniaji Charles Njoroge (Mwenyekiti) na mwaniaji-mwenza Wilfred Mukaka, Martin Karanja (Katibu), Meshack Osero (mhazini), Moses Oduor (mwakilishi wa vijana) na Susan Mudongoi (mwakilishi wa wanawake) ni kati ya wagombezi ambao wamejiondoa.

Sita hao kutoka eneo la Nairobi Magharibi wametaka majina yao kuondolewa katika orodha ya wawaniaji wa nyadhifa za FKF.

“Tunaondoa ugombezi wetu kwa sababu hatuna imani na mchakato mzima ambao kwa sasa unatathminiwa na SDT. Kwa mtazamo wetu, maandalizi ya uchaguzi wa FKF yanaenda kinyume na Katiba ya Kenya (2010), Sheria ya Spoti ya 2013, kanuni za uchaguzi kwa mujibu wa FIFA na Katiba ya FKF ya 2017,” ikasema sehemu ya barua iliyowasilishwa na sita hao kwa Bodi ya Uchaguzi ya FKF.

Wiki jana, Kentice Tikolo ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi ya FKF alithibitisha orodha ya wagombezi na wapigakura waliokuwa wameidhinishwa kushiriki uchaguzi huo ambao umetupiliwa mbali na SDT chini ya mwenyekiti John Ohaga mara mbili katika kipindi cha miezi minane iliyopita.

Uchaguzi huo uliahirishwa kwa mara ya kwanza mnamo Desemba 2019 kisha Machi 2020 kutokana na ukiukwaji wa baadhi ya Sheria za Michezo nchini Kenya za mwaka wa 2013.

Mapema wiki hii, wawaniaji wengine wa kiti cha urais wa FKF – Sam Nyamweya, Alex Ole Magelo, Steve Mburu, Simon Mugo, Twaha Mbarak na Nicholas Musonye waliwasilisha kesi kwa SDT kupinga kuandaliwa kwa uchaguzo ujao wa FKF.

“Wakati umefika kwa FKF kufuata sheria. Klabu zote zinastahili kukubaliwa kupiga kura katika uchaguzi huo na mchakato wa kuamua nani asiyestahili kushiriki kuwekwa wazi kwa wadau wote. Hilo likifanyika, basi tutakuwa radhi kushiriki uchaguzi huo hata kesho,” akasema Nyamweya.

Wengine ambao wamewasilisha malalamiko yao kwa SDT ni Angeline Mwikali anayelenga kuhifadhi kiti cha uanachama wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ya FKF katika eneo la Mashariki na Michael Esakwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa FKF wakati Nyamweya alipokuwa mwenyekiti wa shirikisho hilo kati ya 2011 na 2015.

SDT itasikiliza na kuamua kesi hiyo hapo kesho Ijumaa.

Kwa pamoja na wawakilishi wa klabu za Bondeni na Cheptiret, wawaniaji hao wameishtaki Bodi ya Uchaguzi ya FKF, mwenyekiti wake Tikolo na FKF yenyewe, na wanaitaka SDT kutupilia mbali mwongozo wa uchaguzi uliotolewa na Bodi ya Uchaguzi ya FKF.

“Tunahisi kwamba FKF haiwezi kuandaa uchaguzi wa haki kwa sababu hakuna usawa kwa wagombezi na hata wapigakura kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa. Isitoshe, mwongozo huo unahitilafiana na Katiba ya Kenya na maamuzi ya awali ya SDT,” akasema Nyamweya.

Malalamishi mengine dhidi ya FKF yamewasilishwa na wadau mbalimbali wa soka katika mahakama tofauti za Mombasa, Murang’a, Kericho na Nairobi.

Mnamo Jumanne iliyopita, Tikolo alitangaza kwamba uchaguzi mpya wa FKF ungefanyika Septemba 19 katika kiwango cha kaunti huku wa ule wa kitaifa ukiandaliwa Oktoba 17, 2020. Bodi hiyo ilichapisha orodha ya mwisho ya klabu zitakazopiga kura mnamo Agosti 22.

Maafisa wapya kutoka kaunti 45 watachaguliwa na klabu ambazo zimekuwa zikishiriki mapambano mbalimbali ya soka ya humu nchini kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Nairobi, Kiambu, Kilifi, Mombasa, Kisumu, Migori na Nakuru zitakuwa na idadi kubwa ya wapiga kura hasa ikizingatiwa kwamba zina zaidi ya vikosi 30 kwa pamoja vitakavyopiga kura katika kiwango cha kaunti.

Uchaguzi unatarajiwa kuwa wa haraka katika Kaunti ya Murang’a iliyo na klabu tatu pekee huku Nyeri, Nyandarua, Taita-Taveta na Kirinyaga zikiwa na vikosi vitano kila moja.

Wajumbe 18 wa klabu za Ligi Kuu ya Kandanda humu nchini (FKFPL), 10 wa Ligi ya Kitaifa ya Supa (Betika NSL), 10 wa Ligi ya Daraja la Kwanza, watatu wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake (KWPL) na mmoja wa Ligi ya Wanawake daraja la kwanza; ndio watakaopiga kura katika uchaguzi wa kitaifa.

Uchaguzi wa kaunti utakaofanyika Septemba 19 na ule wa kitaifa mnamo Oktoba 17.