Habari za Kaunti

Sita waugua kwa kunywa maji ya sumu

April 4th, 2024 1 min read

NA KNA

WATU sita wamelazwa hospitalini baada ya kunywa maji ya kisima yanayoshukiwa kuwa na sumu katika kijiji cha Ndemra, Kaunti ya Migori.

Maji hayo yanaaminika kuwa na kemikali aina ya “syenite” kutoka kiwanda kimoja cha madini.

Akiongea katika kiwanda hicho kilichoko katika kaunti ndogo ya Nyatike, Naibu Kamishna wa eneo hilo, Bw Daniel Omukoko, aliamuru kufungwa kwa kiwanda hicho kwa kuwa hakina leseni.

Aidha, aliagiza viwanda vya kutayarisha madini vinavyoendesha shughuli katika kaunti ya Migori bila leseni visalie kufungwa.

Ng’ombe watatu na mbuzi watatu pia walikufa baada ya kunywa maji kutoka kwa kisima hicho.

Bw Omukoko alisema uchunguzi unaendeshwa kuhusu kisa hicho na utakapokamilika, washukiwa watachukuliwa hatua za kisheria kwa kuendesha shughuli bila leseni na kuhatarisha maisha ya watu na mifugo.