Habari Mseto

Sitafuti kiti cha kisiasa, asisitiza Raila

May 11th, 2019 1 min read

Na CAROLINE WAFULA na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amesisitiza kwamba msimamo wake wa kuungana na Rais Uhuru Kenyatta hauna lengo la kumwezesha kurithi urais ifikapo mwaka wa 2022.

Akizungumza Jumamosi katika boma lake la Opoda Farm lililo eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya, Bw Odinga alisema hakuna wakati wowote ambapo wamewahi kutangaza atawania wadhifa wowote wa kisiasa tangu alipoweka mwafaka wa maelewano na Rais mnamo Machi 9, 2018.

“Ajenda yetu pekee ya umoja wetu ni kuwezesha Kenya kuwa na msingi thabiti utakaowezesha taifa kustawi. Huo ndio msimamo wangu na Uhuru,” akasema.

Naibu Rais William Ruto na wandani wake wamekuwa wakimshambulia Bw Odinga kwa maneno wakidai anatumia mwafaka wake na Rais Kenyatta kujitafutia nafasi ya kuingia serikalini Uchaguzi Mkuu ujao utakapofanywa.

Kulingana nao, misimamo mikali inayoshikiliwa na Bw Odinga hasa kuhusu wito wa marekebisho ya katiba na juhudi za kupambana na ufisadi imelenga kuvuruga nafasi ya Dkt Ruto kushinda uchaguzini.

“Sisi huwa hatuzungumzi kuhusu Waluo wala Wakikuyu bali tunaongea kuhusu Wakenya wote. Tunataka kila Mkenya awe na nafasi sawa. Kenya pekee ambayo mimi na Rais tumeelewana kupata ni yenye umoja na utulivu,” akasema.

Alikuwa ametembelewa bomani mwake na sehemu ya wazee wa jamii ya Wakikuyu kutoka Kaunti ya Nakuru wakiongozwa na Mbunge wa zamani wa Molo, Bw Njenga Mungai.

Kuvumisha malengo

Walisema ziara hiyo ni sehemu ya kuvumisha malengo ya handisheki, hasa kuhusu kuleta umoja wa kitaifa kwa jamii zote za nchi.

Viongozi wengine waliokuwepo ni Maseneta Moses Kajwang (Homa Bay), James Orengo (Siaya), Wabunge Elisha Odhiambo (Gem), Otiende Amollo (Rarieda), Millie Odhiambo (Mbita), John Mbadi (Suba Kusini), Opiyo Wandayi (Ugunja) na Gavana wa Siaya, Bw Cornell Rasanga.

Bw Wandayi alikashifu wale wanaopinga juhudi za kurekebisha katiba na handsheki ambayo imesaidia kuleta amani nchini.