HabariSiasa

Sitaki kiti chenu, nitawapa dawa yenu, Weta aiambia ODM

March 26th, 2018 2 min read

Na WYCLIFF KIPSANG

Kwa ufupi:

  • Bw Wetang’ula asema hatahudhuria kongamano la maseneta la kujadili na kutatua masuala yanayotisha kusambaratisha NASA
  • Amshambulia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kudharau eneo la Magharibi licha ya kumuunga mkono kwa miaka mingi
  • Nilidhani hali ingedumishwa lakini nilitusiwa na kudhalilishwa. Matamshi yaliyotolewa yalionekana kuwa yaliyopangwa kuniabisha -Wetang’ula
  • BwMudavadi asema kuna mipango ya vyama vyote vya kisiasa eneo la Magharibi kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

MPASUKO katika muungano wa NASA ulipanuka wazi Jumapili baada ya Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula kukata tamaa ya kupigania kiti cha Kiongozi wa Wachache katika Seneti na kutangaza kwamba hatapigania tena wadhifa huo.

Bw Wetangula alisema hatahudhuria kongamano lililopangwa la maseneta wa NASA la kujadili na kutatua masuala yanayotisha kusambaratisha muungano huo.

“Ni nini cha kujadili (katika kongamano hilo)? Sitahudhuria. Nikienda itakuwa kama kondoo kujipeleka katika mahakama ya fisi,” alisema Bw Wetangula.

“Hata nikipewa kiti hicho sitakichukua, wakae nacho; asante. Sasa mchezo uanze; tutawapa dawa yao polepole lakini hatari sana,” aliongeza kiongozi huyo wa chama cha Ford Kenya.

Alisisitiza kuwa hakuomba kiti hicho cha Kiongozi wa Wachache katika Seneti lakini akiwa mmoja wa vinara wa NASA, uamuzi wa kumpa wadhifa huo ulinuiwa kutia nguvu shughuli katika bunge hilo.

Bw Wetangula alimshambulia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kwa kudharau eneo la Magharibi licha ya kumuunga mkono kwa miaka mingi.

Wiki iliyopita, maseneta wa ODM walimng’oa Bw Wetangula katika wadhifa wa Kiongozi wa Wachache na kumteua Seneta wa Siaya James Orengo kuchukua wadhifa huo. Bw Wetangula alisema Ford Kenya iliungana na ODM kwenye uchaguzi wa 2013 sawa na 2017.

“Tuliweka mali na nguvu zetu kwa suala hili lakini kama jamii ya Mulembe hakuna la kutufaidi,” Bw Wetangula alisema alipohutubia wanahabari mjini Bungoma.

“Imesemekana ninapigwa vita. Ninataka kutangaza hapa na sasa kwamba nina amani katika moyo wangu,” alisema Bw Wetangula.  Alitaja mkutano wa vinara wa NASA na maseneta wa muungano huo Alhamisi kama duka la kelele.

“Nilidhani hali ingedumishwa lakini nilitusiwa na kudhalilishwa. Matamshi yaliyotolewa katika mkutano huo yalionekana kuwa yaliyopangwa kuniabisha,” alisema Bw Wetangula.

Alikuwa ameandamana na kiongozi wa chama cha ANC ambaye ni mmoja wa vinara wa NASA Musalia Mudavadi, Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati na aliyekuwa seneta wa Kakamega, Bonnie Khalwale.

Wengine walikuwa wabunge Wafula Wamunyinyi (Kanduyi), Eseli Simiyu (Tongaren), Ayub Savula (Lugari).

Bw Mudavadi alikosoa mazungumzo kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wa kuwatenga vinara wenza wa NASA.

“Hatupingi mazungumzo lakini tunataka yahusishe watu wote. Hakuna aliye na haki ya kushiriki mazungumzo. Canaan yetu si harambee house, bado tunaendelea mbele, “ alisema Bw Mudavadi.

Hata hivyo, akiongea katika kanisa la CITAM, mjini Rongai Jumapili, Bw Odinga alisema mwafaka wake na Rais Kenyatta ni wa kuunganisha Wakenya.

Bw Mudavadi alisema kuna mipango ya vyama vyote vya kisiasa eneo la Magharibi kuungana kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Maeneo mengine yamefanya hivyo. Sioni sababu yetu kukosa kuungana hapa. Sisi kama viongozi wa Magharibi tunamuunga Bw Wetangula,” alisema Bw Mudavadi.

Alisema walipoungana katika NASA lengo lao lilikuwa mageuzi, kuimarisha uhuru wa asasi za kikatiba na mageuzi ya polisi. “ Tunasikitika kusema kwamba ndoto ya NASA haijatimizwa, nchi yetu inakabiliwa na changamoto tele ikiwa ni pamoja na vijana kukosa ajira,” alisema.