Siasa

Sitawaacha mayatima kisiasa, Gachagua asema ngomeni

February 11th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewaahidi wenyeji na wakazi wa Mlima Kenya kwamba hatawaacha wakiwa ‘pweke kisiasa’, kama alivyofanya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Mnamo Jumamosi, Bw Gachagua alisema kuwa licha ya shughuli zake nyingi za kikazi, amejitwika jukumu la kuangalia na kubaini viongozi ambao wana uwezo wa kuliongoza eneo hilo baada yake kung’atuka uongozini.

Bw Gachagua alitoa kauli hiyo alipozuru Kaunti ya Murang’a, kwenye ziara iliyoonekana kama njia ya kuzima siasa za urithi ambazo zimekuwa zikiendelea katika eneo hilo.

“Mimi si mwerevu sana, japo huwa naangalia mbele. Kile nawaahidi ni kuwa sitawaacha kama mayatima wa kisiasa, kama alivyofanya Bw Kenyatta. Alituacha bila kiongozi rasmi, kwani alikuwa akiwazima viongozi ambao walionekana kuchipuka ili kujaza nyayo zake. Mimi sitafanya hivyo. Nitawalea viongozi, hasa vijana. Nitaangalia na kubaini yule atajaza nafasi yangu, baada ya wakati wangu kuondoka kufika,” akasema Bw Gachagua.

Bw Gachagua alionekana kuwalenga viongozi ambao wamekuwa wakimpendekeza mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) kuwa mgombea-mwenza wa Rais William Ruto, kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

Viongozi wengine walimpendekeza awe mwaniaji urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2032.

Baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakiongoza juhudi hizo ni Seneta Joe Nyutu wa Kaunti ya Murang’a.

Hata hivyo, Bw Gachagua alipuuzilia mbali midahalo hiyo, akisema kuwa huu ni wakati ambapo viongozi wanafaa kuwahudumia raia, badala ya kujihusisha kwenye mashindano ambayo hayawezi kuwafaidi raia.

“Hatujamaliza hata miaka miwili tangu tulipochaguliwa. Huu ni wakati tunaofaa kuutumia kuwafanyia kazi wananchi. Tunafaa kuendesha umoja wa kisiasa ili kuhakikisha eneo hili linafaidika kutoka kwa miradi inayoendeshwa na serikali,” akasema.

Bw Kenyatta amekuwa akilaumiwa kwa kutomtawaza mrithi wake, hali ambayo imechangia eneo hilo kuyumba kisiasa.