Habari

Sitoki KNUT ng'o, aapa Sossion

May 1st, 2018 2 min read

Na WYCLIFFE MUIA

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Walimu nchini (Knut) Wilson Sossion Jumanne alisema hang’atuki kamwe baada ya Baraza la muungano huo kumtaka kutoka kwa wadhifa huo.

Bw Sossion alitimuliwa Jumatatu baada ya wanachama 22 wa Baraza Kuu la Knut (NEC) kupiga kura ya kumuondoa dhidi ya wanachama wawili waliopinga hoja hiyo.

Baraza hilo lilimteua Naibu Katibu Mkuu wa Knut Hesbon Otieno, kuchukua nafasi ya Sossion ili kuhakikisha shughuli za Knut zinaendelea bila kuvurugwa.

Akihutubu wakati wa sherehe za Leba Dei katika bustani ya Uhuru, Nairobi Jumanne, Bw Sossion alisema haendi popote na kuahidi kuendelea kuhudumu kama Katibu Mkuu wa Knut.

“Mimi ni Katibu Mkuu wa Knut, aliyechaguliwa rasmi na walimu wa Kenya,”alisema Bw Atwoli.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Wanyakazi nchini (Cotu) Francis Atwoli aliyeongoza sherehe hizo za Leba Dei, alishutumu Baraza la Knut kwa kumtimua Sossion na kulitaka libatilishe uamuzi huo.

 

Kutumiwa na wanasiasa

“Baadhi ya walimu wanatumiwa na wanasiasa na tutawaonyesha umuhimu wa Sossion kuendelea kuwatetea bungeni akiwa katibu wao mkuu,”alisema Bw Atwoli.

Bw Atwoli alisema Cotu itasimama na Sossion na kuwaonya walimu dhidi ya kusambaratisha Knut kwa kukubali ushawishi wa kisiasa katika masuala ya walimu.

Wanachama wa Baraza la Knut walisema hatua hiyo iliafikiwa baada ya kutolewa kwa ripoti kuhusu mwenendo wa Bw Sossion.

“Sossion alijiondoa mkutanoni na kusema hatashiriki mchakato huo wa kupiga kura ya kumtimua,” mmoja wa wanachama wa baraza hilo aliambia Taifa Leo.

Mkutano huo wa Jumatatu ulihudhuriwa na maafisa wakuu wa Knut akiwemo mwenyekiti Wycliffe Omuchenyi, Naibu Katibu Mkuu Collins Oyuu, Kaimu Mweka hazina Muuo Ndiku, na kaimu mwekahazina Dorothy Muthoni.

 

Kuchaguliwa bungeni

Masaibu ya Sossion yalianza Agosti 2017 wakati Waziri wa Leba na Masuala ya Afrika Mashariki wakati huo Phyllis Kandie, kumtaka Sossion na viongozi wengine10 wa vyama vya wafanyakazi kujiuzulu baada ya kuchaguliwa bungeni.

Bw Sossion aliteuliwa cha chama cha ODM kama mbunge maalum.

Januari mwaka huu, Tume ya Kuuwajiri Walimu(TSC) ilimuondoa Sossion kutoka sajili ya walimu nchini baada ya kuteuliwa bungeni.

Wengine waliotakiwa kujiuzulu ni mwenyekiti wa KUPPET Omboko Milemba ambaye alichaguliwa kuwa mbunge wa Emuhaya.

Knut ina zaidi ya wanachama 200,000 ambao huchanga zaidi ya Sh1.6bilioni kila mwaka kwa muungano huo.