Habari Mseto

Siwezi kuiba mamilioni ya mteja wangu, wakili ajitetea

January 23rd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAKILI alishtakiwa Jumatatu kwa kumwibia mteja wake Sh6.5 milioni alizopokea kwa kuuza shamba.

Bw Simon Shivaji alikanusha shtaka mbele ya hakimu mkazi Bi Hellen Onkwani katika mahakama ya Milimani Nairobi.

Bw Shivaji alidaiwa kati ya Machi 1 na Julai 31 2015 mjini Nairobi alimwibia Bi Nelly Nafula Mutua Sh6,500,000 alipokea kutokana na mauzo ya shamba.

Bw Shivaji ambaye ameondolewa kwa orodha ya mawakili aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana.

Wakili Polycap Owangwae anayemtetea aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema , “ hatatoroka ila afika kortni wakati wa kusikizwa kwa kesi.”

Bi Onkwani alifahamishwa kuwa , Bi Mutua alipeleka malalamishu kwa kamati ya nidhamu ya chama cha mawakili nchini LSK na kumshtaki Bw Shivaji.

“ Kamati ya LSK ilimpata na hatia mshtakiwa na kutoa jina lake katika orodha ya mawakili wanaotambuliwa,”alisema Bw Ongwae.

Mahakama ilielezwa zaidi kwamba kesi hiyo ya Bi Mutua ilipelekwa katika Mahakama kuu na inaendelea kusikizwa.

“Ombi la Bi Mutua sasa linashughulikiwa katika mahakama kuu kupitia kwa kampuni nyingine ya mawakili,” alisema Bw Ongwae.

Hakimu aliombwa amwachilie mshtakiwa kwa kiwango kisicho cha juu mno cha dhamana akisema “ afisi zake zilifungwa na hana mapato yoyote.”

Bi Onkwani alikubalia ombi la mshtakiwa la kuachiliwa kwa dhamana na kumwamuru “ alipe dhamana ya Sh800,000 pesa tasilimu kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani kutoka gerezani.”

Mahakama ilitenga kesi hiyo isikizwe Feburuari 27 mwaka huu.

Upande wa mashtaka uliamriwa umkabidhi mshtakiwa nakala za mashahidi.