Habari za Kitaifa

Siwezi kujiunga na serikali yako iliyojaa uozo, Kalonzo aambia Ruto


KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka amesema hana nia ya kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza akisema hataki kuhusishwa na utawala unaoongozwa na Rais William Ruto.

Bw Musyoka alipuuzilia mbali mazungumzo kwamba upinzani unajiandaa kwa serikali ya umoja wa kitaifa akisema Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya hauna mpango huo.

Akizungumza wakati wa Mkutano wa Baraza la Kitaifa la chama hicho (NEC) katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi Jumatano, Bw Musyoka alisema muungano huo utakutana hivi karibuni na kuweka bayana kwa Raila Odinga kwamba Wakenya hawataki kuhusishwa na utawala wa Kenya Kwanza.

“Raila Odinga, kiongozi wetu wa muungano atatukutanisha na tutamwambia kuwa Wakenya hawataki midahalo kwa sababu kumekuwa na midahalo mingi hapo awali. Hatutaki kuonekana tunasafisha serikali ambayo imefeli,” Bw Musyoka alisema.

Bw Musyoka alishambulia vikali serikali akisema hataki kwa vyovyote vile kuhusishwa na utawala ambao unaandamwa na visa vya mauaji ya kiholela, utekaji nyara na watu kukamatwa kiholela usiku.

“Inaonekana vikosi vya wauaji vimerudi. Utekaji nyara na maafisa wa polisi lazima ukome!”

“Uozo huu uko katika uongozi wa Huduma ya Polisi ambayo sasa imebadilika na kuwa kikosi na sio huduma kama inavyotambua katiba,” alisema.

Akizungumzia kuhusu serikali ya muuungano wa kitaifa kati ya Bw Odinga na Rais Ruto, Bw Musyoka alisema upinzani uko thabiti na kwamba hakuna mjadala kuhusu kujiunga na serikali alioshiriki.

Siku ya Jumanne, Rais Ruto alidokeza kuwepo kwa mpangilio mpana wa kisiasa ambao wadadisi wa kisiasa walitafsiri kumaanisha serikali ya umoja wa kitaifa.

Huku akilaani matumizi ya nguvu kupita kiasi iliyotumiwa na polisi kuzima maandamano ya vijana, Bw Musyoka alisema Azimio hivi karibuni itaitisha mkutano kuangazia masuala yaliyoibuliwa na waandamanaji.

Haya yanajiri Musyoka akionekana kutoa matakwa mapya yanayoweza kuchelewesha miswada ya ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (Nadco)

Bw Musyoka alipokuwa akizungumza wakati wa kupitishwa kwa Mswada wa Marekebisho ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, 2024 alisema kutokana na maandamano yaliyokuwa yakiendelea ya kuipinga serikali, kuna haja ya kuangaliwa upya kwa miswada hiyo.

“Kuna haja miswada minane iliyobaki iangaliwe upya kwani inafaa kuoana na hali ilivyo sasa,” akasema Bw Musyoka.

Kiongozi huyo alisema kuwa suala la kupanda kwa gharama ya maisha liliwasilishwa na mrengo wa upinzani ila likakataliwa na serikali ya Kenya Kwanza na sasa lazima uangaziwe akisema ni miongoni mwa masuala yaliyoibuliwa na waandamanaji wa Gen Z.

“Kama muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, tuliwasilisha suala hilo kwa kamati lakini Bw Kimani Ichung’wah na timu yake ya Kenya Kwanza walitueleza kuwa ni jukumu la serikali kuangazia suala hilo,” Bw Musyoka alisema.

“Ninatumai kwamba kwa kuzingatia maendeleo ya hivi majuzi, rafiki yangu Bw Kimani angerekebisha hilo kwa sababu ya maandamano yaliyochochewa na Mswada wa Fedha 2024,” akaongeza.

Wakati wa mkutano wa Kamati Kuu wa Kitaifa (NEC) Jumatano, uongozi wa Chama cha Wiper ulishtumu utawala wa Kenya Kwanza kwa kukwamisha utekelezaji wa ripoti ya Nadco na kutaka suala hilo liangaziwe kwa haraka.

Akihutubia wanahabari baada ya mkutano huo, Seneta Shakila Abdalla alimsifu Rais William Ruto kwa kuidhinisha IEBC lakini akataka kupitishwa kwa Miswada iliyosalia ili kuipa uhai ripoti ya NADCO.

Seneta Abdalla alisema iwapo Rais Ruto alishughulikia masuala kadhaa yanayowabana Wakenya yakiwemo kupanda kwa gharama ya maisha na kutekeleza ripoti hiyo kikamilifu, basi machafuko na vifo vilivyoshuhudiwa nchini wiki chache zilizopita, yangezuliwa.