Michezo

Siwezi kumzuia Silva kuondoka – Pep

July 21st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Pep Guardiola amesema kwamba hana uwezo wa kumshawishi David Silva kusalia uwanjani Etihad kwa kipindi kingine zaidi licha ya kwamba huduma zake bado zinahitajika zaidi kambini mwa kikosi chake cha Manchester City.

Ushawishi wa Silva ambaye ni kiungo matata mzawa wa Uhispania, umehisika zaidi uwanjani katika kampeni za Man-City msimu huu na ni matarajio yake kwamba atawazolea waajiri wake hao taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kuondoka rasmi mwishoni mwa muhula.

Silva, 34, atatamatisha rasmi kipindi cha miaka 10 akivalia jezi za Man-City mwishoni mwa msimu huu. Tangu aingie katika sajili rasmi ya Man-City mnamo 2010, Silva ambaye anahusishwa pakubwa na klabu za Inter Miami (Amerika), Real Betis (Uhispania), Vissel Kobe (Japan), Al-Duhail (Qatar) na AC Milan (Italia).

“Ameamua kuondoka na hilo ni jambo ambalo amelisisitiza mara nyingi. Nadhani alikuwa na malengo ya kusakatia Man-City kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya kutafuta hifadhi kwingineko. Japo tunamhitaji sana, sioni kabisa akirudi nyuma. Ataagana nasi mwishoni mwa msimu huu na soka ya EPL itamkosa sana,” akasema Guardiola.

Guardiola anatarajia kwamba Silva atarejea baadaye uwanjani Etihad kushiriki mechi itakayowapa mashabiki jukwaa la kumuaga kirasmi kabla ya kuwazia kurejea upya katika kikosi hicho kudhibiti mikoba iwapo atapania kujitosa katika ulingo wa ukufunzi.

Silva amechangia jumla ya mabao 95 tangu awajibishwe kwa mara ya kwanza kambini mwa Man-City mnamo Agosti 2010.

Katika umri wake wa miaka 34 na siku 189, Silva ndiye mwanasoka wa tatu mkongwe zaidi katika historia ya EPL kuwahi kuchangia zaidi ya mabao 10 katika msimu mmoja baada ya Dennis Bergkamp, 35, (2004-05) na Paolo Di Canio, 35, (2003-04).