Habari MsetoSiasa

Siwezi kuwa mwenyekiti wakati magavana wenzangu wananisaliti – Mvurya

January 17th, 2019 2 min read

FADHILI FREDRICK na BERNARDINE MUTANU

GAVANA wa Kwale Salim Mvurya na mwenzake wa Kirinyaga Anne Waiguru wamezungumzia uchaguzi wa Jumatatu huku Mvurya akiwalaumu magavana wenzake kwa usaliti.

Kwa upande wake, Bi Waiguru alipuuzilia mbali hatua ya magavana kutomchagua kama mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) mapema wiki hii.

Bw Mvurya ambaye Jumatatu alitazama mwenzake wa Turkana Josephat Nanok akimtoa nyama mdomoni kwa kuitisha uchaguzi mpya, anasema anahisi vibaya kwamba CoG haikutimiza ahadi yake.

“Kwa maoni yangu hapakuwa na haja ya kuwa na uchaguzi. Baraza hilo mwaka wa 2017 lilifanya uamuzi wa wazi kuwa litapeana uongozi kwa mtu mwingine bila uchaguzi,” akasema akirejelea kikao kilichofanywa Desemba 15, 2017.

Kwenye mkutano huo katika kaunti ya Kwale, magavana walikubaliana kuwa Bw Nanok angekabidhi mamlaka kwa Bw Mvurya kama mwenyekiti mpya katika kipindi cha miezi sita.

Ina maana kuwa, Bw Mvurya alipaswa kuanza kuchukua uongozi wa Baraza hilo la Magavana tangu Juni mwaka 2018.

Hata hivyo, Bw Nanok aliendelea kuwa uongozini hadi Jumatatu, ambapo aliitisha uchaguzi na magavana wakamchagua Bw Wycliffe Oparanya wa Kakamega.

“Kwa hakika hakuna uadilifu wala haki katika CoG. Siamini kwamba baraza hilo linaweza kuenda kinyume na ahadi zake,” akasema nje ya afisi yake mjini Kwale, alipotembelewa na Waziri wa Utalii, Bw Najib Balala.

Kwenye uchaguzi wa Jumatatu, Bw Oparanya aliwashinda magavana Peter Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Anne Waiguru (Kirinyaga) na Jackson Mandago (Uasin Gishu).

Kinyume na taarifa kuwa alikuwa miongoni mwa walioshindwa kwenye uchaguzi huo, Bw Mvurya jana alisema hakushiriki kwenye uchaguzi huo kwa kuwa hakusafiri kwenda Nairobi.

“Sikuona haja ya kwenda kushiriki katika uchaguzi ilhali nilistahili kukabidhiwa uongozi wa CoG kama tulivyokuwa tumekubaliana. Niliamua nikague miradi ya watu wa Kwale ambao ndio waajiri wangu,”akasema.

Baraza la Magavana limekuwa na viongozi wanaojulikana kuwa na misimamo mikali, na huenda ikawa sababu ya Bw Mvurya kutopendelewa na wenzake.

Viongozi waliotangulia; Isaac Ruto, Peter Munya na Bw Nanok wanachukuliwa kuwa watu wenye kukabili matatizo kwa kutumia kifua, kinyume na Bw Mvurya ambaye huonekana mpole na anayesamehe kwa urahisi.

Bi Waiguru alipuuzilia mbali hatua ya wenzake kutomchagua kama mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG).

Akihutubia wasimamizi wa wadi katika taasisi ya mafunzo ya kifedha (KSMS), Gavana Waiguru alisema kilichoendelea wakati wa uchaguzi ulioendelea mapema juma hili ilikuwa ni ‘siasa’.

Aliongeza kuwa ilikuwa hatua ya ‘kawaida’ na kwamba hakukuwa na jambo kubwa lililoendelea.

“Sikuwa nikiwania uenyekiti, nilikuwa nimejiondoa mapema lakini kama katika chaguzi zingine, kulikuwa na washindi na walioshindwa. Baraza lilifanya uamuzi wa kubadilisha mikakati na kwa sababu ya hilo, walihitaji nyuso mpya kutekeleza mikakati hiyo,” alisema.

Hata hivyo, alilalamikia kutokuwepo kwa uwakilishi wa wanawake katika kamati simamizi ya CoG.

“Inasikitisha kwamba hatuna mwanamke yeyote katika kamati simamizi. Sisi ni wachache sana, lakini ninatumainia kwamba hali itaimarika, hatua moja kwa wakati,” alisema Bi Waiguru, ambaye alikuwa naibu mwenyekiti wa baraza hilo.