Michezo

Skendo ya Neymar Jr yaanza kutikisa Brazil

June 14th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

RIO DE JANEIRO, Brazil

BRAZIL inafaa kuwa inajitayarisha kwa soka nyingine ya kifahari kwa hamu kubwa ikiamini mshambuliaji Neymar ataisaidia kumaliza ukame wa miaka 12 bila taji.

Badala yake, nyota huyo, ambaye jeraha la kifundo limemweka nje, anagonga vichwa vya habari kwa sababu zisizofaa.

Neymar anakabiliwa na sakata ya ubakaji dhidi ya mwanamitindo mmoja aliyempata kupitia kwa mitandao ya kijamii katika hoteli moja nchini Ufaransa anakosakata soka katika klabu ya Paris Saint-Germain.

Madai hayo yamechafua hafla hii ya Amerika ya Kusini inayofaa kuwa sherehe na hayaonyeshi dalili ya kuzima, wakati kesi hiyo ya kichuna huyo Najila Trindade Mendes de Souza kutokota.

Ililipuka Juni 2 pale Neymar alichapisha video ya dakika saba kwenye mtandao wake wa Instagram, ambako alipata kumjua Trindade, akifichua kwamba alikuwa akikabiliwa na kesi ya ubakaji.

Sakata hiyo ilienea kwa haraka na siku tatu baadaye, kiongozi mmoja katika Shirikisho la Soka nchini Brazil alibashiri kwamba Neymar atajiondoa katika mashindano haya.

Mvamizi huyo wa PSG alipata jeraha la kifundo katika ushindi wa Brazil wa mabao 2-0 dhidi ya waalikwa Qatar.

Hata hivyo, uwezo wa Brazil kumakinikia shughuli iliyo mbele yake umevurugwa na madai ya ubakaji ya Neymar.

Baada ya Brazil kulimwa 7-1 na Ujerumani katika nusu-fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2014, na mjadala kuhusu kiasi kikubwa cha fedha kilichotumiwa kuandaa soka hiyo pamoja na Olimpiki miaka miwili baadaye, taifa hili lingefaidika bila sarakasi nyingine kama hiyo.

Kocha Tite anasisitiza kwamba Brazil haijaathiriwa kivyovyote kabla ya Copa America, ambayo taifa hilo halijashinda tangu Robinho aliongoze kulemea Argentina iliyokuwa na Lionel Messi 3-0 katika fainali mwaka 2007.

Brazil itafungua kampeni dhidi ya Bolivia mjini Sao Paulo leo usiku. Ilipepeta Honduras 7-0 bila Neymar katika mechi ya mwisho ya kujipima nguvu Juni 9.