Slovakia washangaza Poland kwa kuipokeza kichapo cha 2-1 kwenye gozi la Euro

Slovakia washangaza Poland kwa kuipokeza kichapo cha 2-1 kwenye gozi la Euro

Na MASHIRIKA

SLOVAKIA waliduwaza Poland kwa kichapo cha 2-1 katika Kundi E kwenye fainali za Euro mnamo Jumatatu jijini St Petersburg, Urusi.

Milan Skriniar alifunga bao la pili la Slovakia katika dakika ya 69 baada ya kipa Wojciech Szczesny wa Poland kujifunga katika dakika ya 18 na kuwaweka Slovakia kifua mbele. Slovakia kwa sasa wanashikilia nafasi ya 36 kwenye orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Kujifunga kwa Szczesny kulichangiwa na utepetevu uliomshuhudia akishindwa kulidhibiti kombora aliloelekezewa kiungo mvamizi wa Slovakia, Robert Mak.

Poland walisawazishiwa na fowadi Karol Linetty mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya kusalia na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya kiungo Grzegorz Krychowiak kuonyeshwa kadi ya pili ya manjano kunako dakika ya 62.

Washindani wengine wa Poland na Slovakia kwenye Kundi E ni Uswidi na Uhispania waliotawazwa mabingwa wa Euro kwa mara ya mwisho mnamo 2012.

Poland walitinga robo-fainali za Euro mnamo 2016 ila wakabanduliwa na Ureno walioishia kutawazwa mabingwa kupitia mikwaju ya penalti.

Kikosi hicho kwa sasa kina ulazima wa kupiga Uhispania au Uswidi katika mechi zijazo ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele kutoka Kundi E.

Mak aliyesaidia Manchester City kunyanyua taji la FA Youth mnamo 2008 alipoteza nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo, zingewapa Slovakia idadi kubwa ya magoli katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

Kujifunga kwa Szczesny kuliendeleza masaibu yake kwenye mechi za ufunguzi za Euro. Aliwahi kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi ya kwanza ya Poland kwenye fainali za Euro 2012 kabla ya kupata jeraha baya katika mechi ya ufunguzi wa makundi mnamo 2016 nchini Ufaransa.

Poland hawakuelekeza kombora lolote langoni mwa Slavakia katika dakika 45 kwa kipindi cha kwanza mnamo Jumatatu jijini St Petersburg. Hata hivyo, walifufua makali yao katika kipindi cha pili kupitia ushirikiano mkubwa kati ya Mateusz Klich na Maciej Rubus.

Fowadi Robert Lewandowski aliyefungia Bayern Munich ya Ujerumani jumla ya mabao 48 katika msimu wa 2020-21, alidhibitiwa vilivyo na mabeki wa Slovakia na hakupata nafasi yoyote ya kutambisha Poland katika gozi hilo.

Slovakia walitinga hatua ya 16-bora ya Euro mnao 2016 na ushindi wao dhidi ya Poland unawaweka pazuri zaidi kusonga mbele kutoka Kundi E. Mchuano wao ujao ni dhidi ya Uswidi mnamo Juni 18 uwanjani St Petersburg. Kwa upande wao, Poland watakutana na Uhispania jijini Seville siku hiyo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kituo cha afya kilichotelekezwa Nyeri

Colombia wapepeta Ecuador 1-0 kwenye pambano la kuwania...