Michezo

Slovakia yaondoa Ireland kwenye gozi la kufuzu kwa fainali za Euro

October 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Jamhuri ya Ireland kufuzu kwa fainali za Euro 2021 yalizimwa na Slovakia iliyowapiga 4-2 kupitia penalti kwenye mchujo uliofanyika mnamo Oktoba 8, 2020.

Mshindi wa mechi hiyo iliyochezewa Slovakia aliamuliwa kupitia penalti baada ya pande zote mbili kutoshana nguvu kwa sare tasa mwishoni mwa dakika 90.

Conor Hourihane na Alan Browne walipoteza nafasi mbili za wazi za kufungia Ireland mabao ya ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Penalti ya Browne aliyeshuhudia makombora yake mawili ya kipindi cha kwanza yakigonga mwamba wa lango la wapinzani, ilipanguliwa kirahisi na kipa wa Slovakia, Marek Rodak kabla ya Matt Doherty naye kupoteza penalti yake.

Penalti ya Doherty ambaye ni beki wa Tottenham Hotspur iligonga mhimili wa goli la Slovakia baada ya Hourihane na Robbie Brady kufunga mikwaju yao.

Kuondolewa kwa Ireland kwenye fainali zijazo za Euro ni pigo kubwa kwa kocha mpya Stephen Kenny aliyeaminiwa kuwa mrithi wa mkufunzi Mick McCarthy mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020.

Iwapo wangalipiga Slovakia, Ireland wangalifuzu kuvaana na Northern Ireland katika mchujo wa mwisho utakaosakatwa mjini Belfast mnama Novemba 12, 2020.

Ufanisi kwa Ireland kwenye mechi hizo mbili za mchujo, dhidi ya Slovakia na Northern Ireland, kungaliwapa nafuu zaidi ya kuchezea mechi zao mbili za kwanza za makundi katika uwanja wa nyumbani (Aviva Stadium) jijini Dublin.