Michezo

Sofapaka wavunja benki na kumtwaa beki Kibwage kutoka KCB

September 9th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SOFAPAKA wamewapiku Gor Mahia na vikosi vingine vya haiba kubwa kutoka Zambia na Afrika Kusini katika jitihada za kuwania saini ya kiungo mkabaji wa Harambee Stars, Michael Kibwage.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), wamemsajili Kibwage kwa mkataba wa miaka miwili. Nyota huyo amewahi pia kuchezea AFC Leopards na kupokezwa utepe wa unahodha katika kikosi cha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 23 kambini mwa Harambee Stars.

Sofapaka almaarufu Batoto ba Mungu walianza kumhemea Kibwage baada ya kuambulia pakavu katika juhudi za kumsajili beki na nahodha wa zamani wa Gor Mahia, Musa Mohammed.

Musa, aliyedai kima cha Sh6 milioni ndipo asajiliwe na Sofapaka, kwa sasa hana klabu tangu mkataba wake na mabingwa wa Ligi Kuu ya Zambia (ZSL) utamatike rasmi mnamo Juni 2020.

“Kibwage amejiunga na Sofapaka kwa kiasi kikubwa cha fedha. Tuna furaha kwamba atakuwa sehemu ya kampeni zetu kuanzia msimu ujao. Ni miongoni mwa mabeki wa haiba kubwa watakaoleta nguvu mpya itakayoboresha viwango vya ushindani katika safu ya ulinzi,” ikasema sehemu ya taarifa ya Sofapaka.

Kwingineko, Christopher Oruchum ameapa kutambisha waajiri wake wapya, Tusker FC katika kampeni za FKFPL msimu ujao. Beki huyo aliyeagana na Leopards kwa mkataba wa miaka miwili, anakuwa sajili wa kwanza kuingia kambini mwa Tusker ambao ni mabingwa mara 11 wa KPL.

Oruchum amewahi pia kuvalia jezi za Thika United. Atalazimika kukabiliana na ushindani mkali kutoka kwa Vincent Ngesa, Gabriel Wandera, Eugene Asike na Mganda Rodgers Aloro katika kikosi cha kwanza.

Hadi kampeni za KPL katika msimu wa 2019-20 zilipotamatishwa ghafla kwa sababu ya janga la corona mnamo Aprili 2020, Tusker wanaonolewa na kocha Robert Matano, walikuwa wamepiga jumla ya michuano 15 bila kushindwa.

Wakati uo huo, Nairobi City Stars wamekamilisha usajili wa kiungo Sven Yidah kutoka Kariobangi Sharks kwa mkataba wa miaka miwili.

Yidah aliyekuwa akiviziwa pia na Yanga SC kutoka Tanzania, anakuwa mchezaji wa sita kuingia kambini mwa City Stars muhula huu baada ya Erick Ombija (Gor Mahia), Rowland Makati (Vapor Sports), Timothy Ouma (Laiser Hill Academy), Ronney Kola Oyaro (Kenya School of Government) na kipa Elvis Ochieng Ochoro (Hakati Sportiff).

Yidah ambaye pia huchezea Harambee Stars U-23, anaungana na wanasoka Ebrima Sanneh, Shittu Salim Abdalla na Wycliffe Otieno waliowahi kucheza pamoja naye katika kikosi cha Sharks.

Tangu msimu wa 2017, Yidah ambaye kwa sasa atavalia jezi nambari 18 mgongoni, alichezea Sharks jumla ya michuano 97 kwenye kampeni za KPL.