Michezo

Sofapaka yabandua Tusker SportPesa Shield

September 2nd, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

SOFAPAKA imeingia nusu-fainali ya Soka ya SportPesa Shield baada ya kutoka nyuma bao moja na kuzamisha Tusker 2-1 uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Jumapili.

Jackson Macharia alifungia Tusker ya kocha Robert Matano bao la ufunguzi dakika ya tano baada ya kumegewa pasi nzuri na Boniface Muchiri. Hata hivyo, uongozi huu haukudumu kwani Mganda Umar Kasumba alisawazishia mabingwa wa mwaka 2007, 2010 na 2014 Sofapaka dakika tatu baadaye. Ezekiel Okare alifunga bao lililobandua nje mabingwa mara nne Tusker katika dakika ya 75.

Sofapaka inaungana na mabingwa watetezi AFC Leopards, ambao wameshinda kombe hili la ngao mara nane, na Ulinzi Stars katika nusu-fainali. Leopards na Ulinzi zililemea Kenya Police na Riverplate kwa mabao 4-1 uwanjani Bukhungu mjini Kakamega mnamo Jumamosi.

Mshindi wa mashindano haya hufuzu kuwakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho la Afrika. Leopards ilibanduliwa nje na Fosa Juniors ya Madagascar katika makala ya mwaka huu katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza. Sofapaka na Ulinzi zilishiriki mashindano ya Afrika mara ya mwisho mwaka 2015 na 2017, mtawalia.

Ulinzi ilitolewa katika raundi ya kwanza na Smouha kutoka Misri kwa jumla ya mabao 4-3. Ilifuzu kukutana na Smouha baada ya kulemea Al-Hilal Benghazi ya Libya kwa njia ya penalti 5-4. Sofapaka ilicharazwa 4-2 na Platinum ya Zimbabwe katika mechi ya kuingia raundi ya kwanza.