Michezo

Sofapaka yanasa saini za Roy Okal na Kevin Omondi

August 19th, 2020 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

KLABU ya Sofapaka FC imethibitisha kunasa saini za Roy Okal na Kevin Omondi kutoka Mathare United na Wazito FC mtawalia.

Kiungo Okal na kipa Omondi wamesajiliwa kwa mikataba ya miaka miwili kila mmoja.

Okal mwenye umri wa miaka 24 alikuwa mwanafunzi wa Laiser Hill ambaye alionyesha umaarufu wake wakati wa mashindano ya kitaifa ya shule za sekondari ambapo anatarajiwa kujaza nafasi ya Cercidy ‘Carrick’ Okeyo ambaye ameyoyomea Mashariki ya Kati baada ya mkataba wake na Sofapaka kumalizika.

Mbali na Mathare United hapo awali, Okal aliwahi pia kuchezea Ushuru na klabu moja ya Ugiriki ya daraja la chini.

Omondi kwa upande wake atajaza nafasi ya kipa Mganda, Nicholas Sebwato aliyeondoka baada ya mkataba wake kumalizika, lakini atalazimika kuwania nafasi na Richard Aimo pamoja na Isaiah Wakasala.

Omondi aliyejiunga na Sofapaka akitokea Wazito, awali aliwahi kuchezea SoNy Sugar.