Michezo

Sofia Calzetti arudi kumpa Aguero asali

June 25th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WIKI chache baada ya Sergio Aguero kufichua mpango wa kumfanya mwanamuziki maarufu mzawa wa Argentina, Martina ‘Tini’ Stoessel kuwa wake wa halali, mrembo Sofia Calzetti amekiri kurudiana na mwanasoka huyo wa Manchester City.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Sofia alipakia mtandaoni picha alizopigwa kwa pamoja na Aguero walipokuwa wakiponda raha katika Kisiwa cha Sardinia, Italia na kusisitiza kwamba kubwa zaidi katika matamanio yake ni kufunga pingu za maisha na sogora huyo na kumzalia watoto watakaompanulia familia.

Aguero ambaye pia amewahi kukiri kutoka kimapenzi na kahaba Taylor Ward, alidhihirisha ukomavu wa penzi lake kwa Sofia baada ya kuonekana wakibusiana peupe katika hafla ya kuadhimisha miaka 23 ya kuzaliwa kwa mrembo huyo aliyeandamana na mamaye mzazi.

Aguero aliwahi kufunga pingu za maisha na binti wa Diego Maradona, Gianinna na wakajaliwa mtoto wa kiume kwa jina Benjamin kabla ya ndoa hiyo kusambaratika mnamo 2012.

Nyota huyu alianza kumtambalia Sofia kimapenzi miezi michache tu baada ya kutemana mwanzo na Taylor, 21 aliyehusiana naye kwa siri kisha Tini ambaye ameapa kuwasha upya mwenge wa penzi lake kwa sogora huyo matata wa timu ya taifa ya Argentina.

Kabla ya kupata hifadhi ya penzi lake moyoni mwa Aguero, Sofia aliwahi pia kumfungulia mzinga wake mwigizaji Sam Reece, 26, kabla ya tunda lake kumenywa na beki wa Everton, Mason Holgate, 22.

Baada ya kuzidiwa na baridi ya upweke tangu atemwe na kichuna Karina Tejeda mnamo 2018, Aguero alianza kuburudishwa na mwanamitindo mzawa wa Italia, Zoe Cristofoli aliyewahi pia kutoka kimapenzi na Andrea Ceroli na mwanahabari Fabrizio Corona. Ceroli ni mshindi wa zamani wa shindano la Big Brother.

Zoe alianza kumfungulia Aguero buyu lake la asali mnamo Oktoba 2018, mwezi mmoja baada ya mvamizi huyo kuhusika katika ajali ya barabarani jijini Amsterdam, Uholanzi. Aguero mwenye umri wa miaka 31 alilidokoa tunda la Karina, 34, kwa miaka minne kabla ya kuachana. Karina ana mtoto mmoja, Sol aliyepatikana katika uhusiano wake wa awali na dume jingine.