Michezo

Sogora mwingine wa Wazito FC astaafu na kupokezwa majukumu katika benchi ya kiufundi

September 22nd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SOGORA mwingine wa Wazito FC, Eric ‘Ero’ Odhiambo amestaafu usakataji wa soka na anatarajiwa sasa kuingia katika benchi ya kiufundi ya mabwanyenye hao.

Odhiambo alitangaza kustaafu kwake, siku chache baada ya mkongwe David Oswe pia kuangika daluga zake. Oswe sasa ameteuliwa na Wazito kuwa menejea msaidizi wa kikosi hicho.

Odhiambo ni miongoni mwa wanasoka ambao wamehudumu kambini mwa Wazito kwa kipindi kirefu zaidi tangu Disemba 2012. Alikuwa sehemu muhimu katika kampeni za kupanda ngazi kwa kikosi hicho kutoka ligi za chini hadi Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2017.

“Imekuwa miaka mingi ya kuonewa fahari ndani ya jezi za Wazito. Ninashukuru wasimamizi wa kikosi hiki kwa kuniamini na kunipa malezi bora ya kitaaluma,” akatanguliza Odhiambo.

“Hata hivyo, nahisi kwamba wakati wa kuondoka ulingoni, kukabiliana na changamoto mpya katika ngazi nyingine na kuwapisha chipukizi wanaoinukia katika soka umewadia,” akasema.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mtendaji wa Wazito FC, Dennis Gicheru alisema: “Odhiambo ni kati ya wanasoka wenye nidhamu ya kiwango cha juu zaidi kuwahi kuchezea Wazito. Klabu nyingi zimekuwa zikiwania huduma zake kwa muda mrefu. Lakini aliteua kusalia kambini mwa Wazito na ameiwajibikia klabu kwa kujituma mno.”

“Ukurasa wa Odhiambo katika usakataji wa kabumbu umefungwa. Wazito kwa sasa watamfungulia ukurasa mwingine katika ngazi tofauti. Atasalia kuwa sehemu ya familia pana ya kikosi hiki cha KPL. Asante sana Odhiambo kwa miaka minane ya kujitolea. Uaminifu wako kambini mwa Wazito utatambuliwa,” akasema Rais wa Wazito FC, Ricardo Badoer.

Baada ya kustaafu wikendi iliyopita, Oswe alipokezwa majukumu ya kuwa meneja msaidizi wa timu chini ya nahodha wa zamani wa klabu ya Wazito FC, Dan Odhiambo. Kiungo huyo mkabaji amekuwa akivalia jezi za Wazito FC kwa miaka saba iliyopita.

“Oswe amekuwa mwaminifu sana kwa klabu kwa kipindi cha miaka mingi. Tumeamua kumpa jukumu la kusimamia kikosi katika benchi ya kiufundi.”

“Hapa Wazito, sisi hutambua na kutuza uaminifu na kwa kujitolea kwake kwa kipindi hicho chote, tumeamua kumpa Oswe majukumu mengine baada ya kuangika daluga zake,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Gicheru.

Kwa upande wake, Oswe alisema: “Safari yangu na Wazito FC imekuwa ya kuonewa fahari. Ingawa tumekuwa na nyakati nzuri na za kusikitisha, tulipoteza na kushinda kama timu nzima. Sasa nahisi kwamba muda umefika wa kuondoka ulingoni na kuwapisha chipukizi kuendeleza mambo mazuri tuliyoyaanzisha kambini mwa Wazito.”

Oswe pia alishukuru usimamizi wa Wazito FC kwa kumwaminia nafasi ya kusimamia kikosi na akaahidi kujitahidi vilivyo kutambisha waajiri wake jinsi alivyofanya kwa uaminifu tangu 2013.

“Ningependa kumshukuru Rais wa Wazito, Badoer na Afisa Mkuu Mtendaji kwa kuniteua kuwajibikia kikosi katika nafasi hii. Naelewa falsafa ya kikosi na matarajio ya klabu kutoka kwangu,” akasema.

Eric Odhiambo akichezea Wazito FC dhidi ya FC Talanta Machi 5, 2017, katika uwanja wa Camp Toyoyo, Jericho ambapo Wazito ilishinda 1-0. Picha/ Chris Omollo