Makala

SOKA MASHINANI: Timu ya Destiny FC yazidi kujikaza kisabuni kwenye Ligi

June 4th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUMEKUWA na hali iliyozoeleka ya kudharau timu za mashinani licha ya kwamba huko ndiko chimbuko la wanasoka ambao huibuka kuwa na sifa tele hapo baadaye.

Destiny FC ni timu katika mtaa wa Makongeni, Thika, na wachezaji wake wengi ni wazaliwa wa mtaa huo na vitongoji vyake.

Kulingana na kocha wake Brian Obembo, timu hiyo ni ya kitambo kwani ilibuniwa mwaka wa 2000.

“Timu hii imekua baada ya msukosuko wa mwaka 2006 uliosababisha ivunjike kutokana na matatizo ya hapa na pale. Timu ilifufuliwa mwaka wa 2009 na wanasoka kadha waliojiunga pamoja tena,” anasema Kocha Obembo.

Kocha wa Destiny FC, Brian Obembo. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema yeye alikuwa mmoja wa wachezaji chipukizi wa klabu hiyo ilipofufuliwa ambapo alicheza kama kiungo kwenye timu hiyo.

Ilipofika mwaka wa 2016 alipokea mikoba ya kuendesha timu hiyo kama kocha mkuu ambapo kwa sasa timu hiyo inashiriki katika Aberdare Regional League ambapo iko katika Kundi A.

Kocha Obembo anajigamba kuwa msimu huu atakipanga kikosi thabiti kuonyesha mchezo wa kufa mtu na kuhakikisha kimevuna matokeo mazuri kwenye ligi hiyo.

Anasema kwa sasa timu yake inakamata nafasi ya tatu na alama 28 huku akiwa nyuma ya Muchatha na Kabati Youth, zikiwa na pointi 34 na 29 mtawalia.

Anasema tangu achukue usukani katika klabu hiyo miaka minne iliyopita amefanya bidii kuwaweka pamoja vijana wake huku akijivunia kuwa na kikosi cha wachezaji 25.

Matokeo mazuri

Hata hivyo, anadokeza kuwa vijana hao wamejitolea mhanga kuona ya kwamba wanapambana na timu hizo bila kuhofia lolote ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wao.

Obembo anawaomba wafanyabiashara na wahisani wa Thika, wajitokeze kuisaidia klabu hiyo na fedha na vifaa ili wapate kufanya vizuri kwenye ligi hiyo msimu huu.

Wachezaji wa klabu hiyo ni makipa Nathan Asira na Peter Odhiambo.

Wengine ni Paul Kimani, Larry Odhiambo, Denis Ngigi na Hussein Seif.

Katika kiungo kuna Gilbert Naraka, Fred Odhiambo, na Edwin Sherrif.

Mastraika ni Tonny Jaoko, na Edwin Chege.

Maafisa wanaoendesha klabu hiyo ni mwenyekiti Wyclife Ochieng’, Katibu ni Bob Dismas, halafu mlezi ni Fred Odhiambo.

Anasema mazoezi wao huyafanyia katika uwanja wa shule ya msingi ya Kamenu mjini Thika kati ya Jumanne na Jumamosi.

“Mimi nimejitolea kunoa vijana hao kwa kujitolea kwa sababu silipwi na yeyote hata senti moja, lakini mashabiki wananipa motisha nizidi kuendelea na msimamo huo,” anasema Obembo.