Michezo

SOKA MASHINANI: Kalimoni FC

July 10th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUMEKUWA na dhana potovu ya kudharau timu za mashinani lakini ni huko hasa ndilo chimbuko la wanasoka wenye ujuzi tele.

Kalimoni FC ni timu ambayo shughuli zake ni za eneo la Juja katika Kaunti ya Kiambu, na wachezaji wengi ni wa mitaa ya hapo.

Kocha wa Klabu hiyo Benard Maina, anajigamba kuwa anacho kikosi cha vijana 25 ambao kwa mtazamo wake wameiva vilivyo.

“Tayari vijana wangu wanafanya vizuri katika mechi za kuwania mataji na zile za kirafiki. Iwapo watajibidiisha wanaweza fika mbali,” alisema kocha Maina.

Anaongeza kuwa tangu abuni klabu hiyo miaka minne iliyopita, hajarudi nyuma bali amefanya bidii kuwaweka pamoja vijana wa umri kati ya miaka 15 hadi 24, wakiendeleza vipaji vyao.

Hata hivyo, anasema kuwa vijana hao wamedhamiria kupambana bila hofu ili kuhakikisha wamepata matokeo mazuri katika mechi zao za kirafiki na kuwania mataji wakijiandaa kwa Ligi ya Kaunti ndogo ya Thika msimu ujao wa 2020.

Katika mechi za hivi majuzi walizocheza za kirafiki Kalimoni FC iliifyeka Ndarugu Stars kwa mabao 3-0 na kuiponda Kiaora FC kwa mabao 2-1.

Hapo awali walitoka sare na Muchatha Youth kwa kulimana 1-1.

Lakini walipoteza mechi yao dhidi ya Gachororo FC ambapo walilazwa mabao 2-1.

Kujiongeza ujuzi

Anasema vijana wanaendelea kujiongeza ujuzi zaidi na kufahamu mchezo huo kwa vile wametambua kuwa soka ina nafasi kuu ya kuwainua kimaisha.

Anasema timu hiyo hufanya mazoezi katika Uwanja wa Premier Bag, Juja kati ya Jumatatu na Ijumaa, na wengi wao bado ni vijana wa shule ambao pia ni sharti wazingatie masomo yao.

“Mimi pia huwashauri wafanye bidii katika masomo yao kwani unapopata elimu tosha uongeze na ujuzi wa soka, bila shaka maisha yako yanaomarika,” anasema Maina.

Anatoa mwito kwa wahisani na wafanyabiashara wenye nia njema wajitokeze hadharani kuona ya kwamba wanainua timu ya Kalimoni.

“Tayari tumewafikia watu hao na kuwapa malilio yetu ambapo wametupatia matumaini kuwa watafanya jambo,” alisema Maina.

Maina anasema kuna vijana wengi wenye vipaji hasa mitaani na kile wanachohitaji ni kuwasaidia wavikuze vipaji hivyo na kupewa mwongo ufaao.