Michezo

SOKA MASHINANI: Klabu ya Thika Sporting FC

June 7th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KIKOSI cha Thika Sporting FC kinakamilisha klabu ambayo imejitokeza hivi karibuni kufanya makubwa licha ya kupitia changamoto tele.

Ni miongoni mwa timu zenye makazi yake katika mtaa wa Makongeni mjini Thika, Kaunti ya Kiambu.

Kocha wa klabu hiyo, Wilson Ndung’u, amekusudia kunoa talanta za wanasoka chipukizi angalau kuimarisha viwango vya mchezo wao ili kukabiliana na timu zingine kwenye ligi.

Kocha huyo anasema kuwa timu hiyo ni ya wachezaji wapatao 28 na lengo lake kuu ni kuona ya kwamba anawasaidia kuwaleta pamoja kupiga chenga mtindo wa kujihusisha na matendo maovu mitaani.

Kulingana na kocha Ndung’u, timu hiyo ilibuniwa mwaka wa 2013 ikiwa na vijana chipukizi waliokuwa na umri chini ya miaka 15 na yeye ndiye mwanzilishi wa klabu hiyo.

“Kwa wakati huu tunashiriki katika Ligi ya Kaunti ndogo ya Thika ambapo tunajivunia kuwa kwenye nafasi ya sita na alama 11. Lakini tunaelewa kuwa tunacho kibarua kikubwa mbele yetu ili tufanikiwe,” anasema Ndung’u.

Anasema timu hiyo hufanyia mazoezi yake katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Kimosho, Kiganjo, Thika.

Anasema eneo la Makongeni, Kiganjo na vitongoji vyake lina vijana wengi wenye vipawa ambao wakipewa mwongozo bila shaka wanaweza kufanya maajabu.

“Ningetaka kusema ya kwamba hapa Makongeni kuna vijana wengi wazuri na wanao uwezo wa kucheza soka safi, lakini shida ni kuwa hamna wa kuwafikisha kule juu,” anasema Ndung’u.

Anakitaja kikosi chake kuwa kinajumuisha kipa Brian Kariuki, madifenda ni Eddy Wanjala, Geoffrey Ouma, na Eric Omondi.

Katika kiungo kuna Kevin Odongo, Denis Mwaura, na Stanely Maina nao mastraika ni Steve Macharia na Jeremiah Marvin.

Maafisa

Maafisa wengine wanaosaidia klabu hiyo kunawiri ni mwenyeki Chrispus Njenga, Katibu Wilfred Gathuka, halafu mlezi ni Kevin Odongo.

Kwa jumla anawashauri wanasoka chipukizi kuzingatia na kumakinika mazoezini ili kuboresha talanta zao.

Anatoa mwito kwa maafisa waliopewa majukumu ya kukuza spoti wafanye hima kwa kujituma na kuona ya kwamba wamefanya jambo.

“Ikiwa eneo hili linaweza kuangaziwa kimichezo na washikadau kujitokeza kuona ya kwamba vijana wanapata vifaa vya michezo, kwa kweli tutapiga hatua ya kipekee,” anasema Ndung’u.

Anazidi kujitetea kuwa kwa sasa kile wanachokosa ni kupata mdhamini ambaye anaweza kuwapiga jeki ili wapate vifaa muhimu vya michezo.

“Kile kinachoponza juhudi zetu sana ni ukosefu wa usafiri tunapokwenda kucheza mechi za Ligi. Wakati mwingi mashabiki, wazazi wa wachezaji ndio hujitolea kuchanga kitu kidogo walicho nacho,” anaeleza Ndung’u.