Michezo

SOKA MASHINANI: Wazee FC ya Thika yataka kuinua vijana

July 7th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

TIMU ya Wazee FC ya Thika inaendelea kujiimarisha kwa kupiga mechi za kirafiki na kukuza talanta za vijana chipukizi.

Mlezi wa timu hiyo Peter ‘Mjoh’ Njoroge, ambaye ni mchezaji wa timu hiyo anasema licha ya kustaafu kutoka kwa soka miaka michache iliyopita, lakini bado wao hutesa timu kadha wanazokutana nazo katika mechi za kirafiki.

Anasema kwa sababu kila mchezaji anaishi katika maeneo tofauti mjini Thika na vitongoji vyake, wao hujumuika katika uwanja wa Safaricom Foundation mjini Thika ili kufanya mazoezi kila Jumanne na Ijumaa.

“Sisi kama wajuzi wa soka, cha muhimu kwetu ni kuona ya kwamba tunajiweka fiti kiafya ili tunapokutana na timu kadha tunaonyesha umahiri wetu uwanjani,” alisema Njoroge kwenye mahojiano na Taifa Leo.¬†

Alisema kikosi chao cha wachezaji wapatao 27 kinahakikisha afya inatunzwa na hawadhoofiki.

Alisema tangu wabuni timu hiyo miaka mitatu iliyopita wamekuwa wakizitesa timu kadha wanazokutana nazo katika mechi za kupimana nguvu.

Kwa mfano anasema hivi majuzi timu ya Wazee FC iliichabanga Roysambu FC kwa mabao 3-2 katika mechi safi iliyopigiwa katika uwanja wa Safaricom Foundation.

Timu hiyo iliendelea kutesa timu kadha pale ilipoizaba Black Spear FC ya Kiambu Road kwa mabao 8-7.

Matokeo hasi ni pale  Thika Islamic FC iliwagonga Wazee FC kwa mabao 4-2. Nayo Nanyuki FC iliibwaga Wazee magoli 2-1.

Maono

Nahodha wa timu hiyo Timothy Wahome, anawahimiza maafisa wanaosimamia soka eneo la Aberdare wawe na maono wakati wa kuendesha maswala ya soka.

“Tunapata ya kwamba wanasoka wengi wenye talanta kutoka Thika wanachezea timu za kitaifa jijini Nairobi. Hata hivyo ni vyema tupate vijana wengi kutoka hapa na wapewe mwongozo ufaao,” alisema Wahome.

Alisema Timu ya Wazee ina maono makubwa licha ya kucheza soka ya kujiburudisha.

“Tungetaka kukuza soka ya vijana hapa Thika na vitongoji vyake. Tungetaka kupata ukumbi mkubwa wa kuwaleta pamoja vijana hawa ili waweze kukuza vipaji vyao,” alisema Wahome na kuongeza hii inataka ushirikiano mkubwa miongoni mwao.

Alisema kati yao katika kikosi hicho kuna vikundi tofauti, ambapo kuna wafanyabiashara, walimu, madaktari na wafanyakazi kutoka sekta nyinginezo.

“Kwa hivyo, tukiunganisha ujuzi huo wote tunaweza kuwapa vijana mwongozo wa kujivunia siku za usoni,” alisema Wahome.

Kikosi cha Wazee kinajumuisha wachezaji kama Patrick Irungu, James Kinyua, George Maina (Kocha), na Erick Kinuthia.

Wengine ni Peter ‘Mjoh’ Njoroge, Timothy Wahome (Nahodha), Andrew Mahinda (Katibu), James Kagondu na Dancan Magere.

Pia kuna Denis Kiprich, Wyclif Utility, Saeed Abdi Saleh na Abdul Kadir.

Wengine ni Stephen Ndung’u, Brian Kamande , Henry Kimani, James Legend, na Patrick Irungu (Mukora).

Kwa sasa wanataka kushirikiana na maafisa wa FKF tawi la Aberdare ili kufanikisha malengo yao ya kuinua soka katika eneo hilo.