Michezo

SOKA: RSM yatafuta chipukizi wenye vipaji na kufanikisha majaribio na klabu mbalimbali za barani Ulaya

May 21st, 2020 3 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KAMPUNI ya Regional Sports Management (RSM) iliyoko Abu Dhabi huko Arabuni imepania kuhakikisha wachezaji wanaoinukia na vipaji katika mataifa mbalimbali barani Afrika wanapata fursa ya kuinua vipaji vyao.

Pia inawasaidia vijana hao kuhakikisha wanasajiliwa na klabu mbalimbali za soka ya kulipwa huko ng’ambo na hasa Bara la Ulaya.

Mapenzi yake kwa mchezo wa soka yalimfanya Omar Al Dhiyebi aanzishe kampuni ya RSM ambayo anaitumikia kutafuta chipukizi wenye vipaji na kuwasaidia kuwapeleka huko Ulaya kwa majaribio.

Omar Al Dhiyebi, meneja wa kampuni kubwa ya Aldar ya Abu Dhabi huko Arabuni alikuwa na hamu ya kuona vijana wanaoinukia vizuri kisoka kwao na barani Afrika ikiwemo nchini Kenya, wanapata fursa ya kwenda kufanyia majaribio na klabu mbalimbali za barani Ulaya.

‘Nilipokua nainukia, nilikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchezaji wa kulipwa lakini hakupata fursa ya kutimiza ndoto yangu hiyo. Nikaamua kuanzisha kampuni ya kuwasaidia vijana wenye talanta wa sehemu mbalimbali za dunia kupata fursa ya kuchezea huko Ulaya,” akasema Omar.

Lengo kuu la Omar ni kuisaidia jamii ya watoto mbalimbali na kuwaondoa mitaani na kujiepusha na tabia mbaya ya na badala yake kuwapa fursa ya kucheza soka la kulipwa ili wapate kujikimu kimaisha.

“Nia yangu kubwa ni kuhakikisha nawasaidia vijana wenye talanta wanapata fursa ya kuonyesha vipaji vya uchezaji wao na kutimiza ndoto zao za kuwa wanasoka wa kulipwa kwa kuchezea timu kubwa duniani,” akasema mmiliki wa RSM.

Kwa upande wa nchi ya Kenya, RSM inasubiri janga la corona limalizike ili waendeleze mikakati yao ya kuwatuma wanasoka kadhaa kutoka jimbo la Pwani kwa majaribio huko Abu Dhabi ambapo watakaofuzu watapelekwa nchi kadhaa za barani Ulaya kujaribvu bahati zao.

Kwa wakati huu, mipango inafanywa ya kiungo mshambuliaji wa Mvita Youngsters FC Abdulrahman Mohamed Miraji ya kusafiri hadi Uhispania kufanyiwa majaribio na klabu za huko ambazo zingali zinawasiliana na kampuni hiyo.

Abdulrahman Mohamed Miraj anatarajia kwenda Uhispania kwa majaribio. Picha/Abdulrahman Sheriff

“Kampuni yetu ya RSM imewasiliana na klabu kadhaa za huko Uhispani juu ya majaribio ya Miraji, tuna matarajio atafuzu kusajiliwa na klabu huko Uhispania,” alisema mwakilishi wa kampuni ya Regional Sports Management (RSM) barani Afrika, Hamid Shariff Ahmed.

Mbali na mipangilio ya Miraji na mwenzake beki Alex Oyata, RSM pia iliteua wanasoka wengine 10 kwenye majaribio iliyoyafanya uwanja wa Mombasa Sports Club mwaka uliopita ambao nao wanafanyiwa mipango ya kuwapa fursa kwenda Ulaya kwa majaribio.

Chipukizi hao waliotoka klabu mbalimbali za Mombasa na eneo zima la Pwani ni Khalid Hassan Mohamed almaarufu Messi, Abubakar Fadhil, Ali Twaha, Suleiman Juma Mwinyikai almaarufu Pogba na Hamadi Mohammed. Pia walo Hassan Noor, Ateek Zubeir Said, Ahmed Swabri na Suleiman Juma Mbaruk.

Vijana hao walifanyiwa majaribio na kocha Mwingereza Kevin Hudjson wakati alipofika Mombasa Julai mwaka uliopita kwa hisani ya RSM kutoa mafunzo kwa makocha pamoja na kuwafanyia majaribio chipukizi wa umri wa miaka 15-18.

Makocha wa Mombasa katika hii picha ya pamoja baada ya kupata mafunzo kutoka kwa Kevin Hudjson aliyedhaminiwa na Regional Sports Management (RSM). Picha/ Abdulrahman Sheriff

Akiongea kwa njia ya simu kutoka Abu Dhabi, Hamid alisema kampuni hiyo ya RSM inafanya bidii kuona wanasoka wenye vipaji barani Afrika hawapotezi vipaji vyao kwa kucheza soka katika nchi zao bali wanafaulu kutimiza ndoto zao za kucheza soka la kulipwa ng’ambo.

“Tungelipendelea washika dau wa soka wa nchi za Afrika na kwetu Kenya serikali kuu na serikali za kaunti pamoja na wahisani washirikiane na kampuni hiyo kusaidia chipukizi waweze kwenda ng’ambo kwa majaribio watizimize ndoto zao za kucheza soka la kulipwa,” akasema Hamid.

Akiwa mzaliwa wa Kenya aliyezaliwa mjini Mombasa, Hamid anasema mwambao wa Pwani una wanasoka wanaoinukia vizuri na wenye kucheza soka la hali ya juu lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa kuinua zaidi vipaji vyao.

Amesema ikiwa serikali ya Kenya na zingine za barani Afrika zitashirikiana na kampuni yake, kutatoka wachezaji wengi wenye vipaji ambao wataweza kufanikiwa kucheza soka la kulipwa ambapo watakuwa wakijisaidia na kusaidia familia zao katika kupeleka maisha yao.

Kocha wa Mvita Youngsters FC, Fahad Abdulaziz alisema wanaishukuru sana kampuni ya RSM kwa kuangazia wachezaji wenye vipaji kutoka mashinani na kuwafanyanyia mipango ya kuwafanyia majaribio na halafu kuwafanyia mipango ya kuwapeleka kwa majaribio nchi za Ulaya.

“Wachezaji kadhaa wa timu yangu ni miongoni mwa wale ambao wanaangaziwa na kampuni hiyo na akawa na matumaini kwa wahisani wa hapa nchi watajitokeza kusaidia vijana wengi zaidi kujiunga na kampuni hiyo katika kuwapa fursa kucheza soka la kulipwa.

“Nina imani kubwa wachezaji waliofanyiwa majaribio na kampuni hiyo watapata fursa za kusajiliwa na klabu za soka za barani Ulaya nan i juu ya viongozi wetu watumie fursa ya kuwasaidia vijana wetu kupitia kwa RSM wafanikiwe kwa lengo lao hilo,” akasema Abdulazi.