Michezo

SOKA SAFI AU MATOKEO? Kiini cha Mourinho kukaangwa na wanahabari kuliko makocha wengine

August 29th, 2018 3 min read

Na PETER MBURU

KOCHA wa Manchester United Jose Mourinho Jumatatu aliondoka kutoka kikao na wanahabari kwa hasira, baada ya kukabiliwa na maswali makali kuhusu kushindwa kwa Man U, wakati wa mechi dhidi ya Tottenham Hotspur.

Katika mahojiano hayo, Mourinho alikuwa kipaumbele kutetea mchezo wa timu yake, akiwataka waliomuuliza maswali kuamua ikiwa wanapenda ubora wa mchezo ama matokeo.

Hoja yake ilikuwa kuwa katika mechi hiyo, Man U ilionyesha mchezo mwema na wa ustadi na alifaa kuheshimiwa kwa mataji aliyoshinda kwenye taaluma yake.

Lakini alilemewa alipoanza kueleza kuwa mashabiki wa Man U walisapoti timu hiyo, licha ya kuwa ilipata kipigo cha ajabu ikiwa nyumbani.

“Unajua hii inamaanisha nini , inamaanisha tulipigwa 3-0, lakini pia inamaanisha nimeshinda ligi ya EPL mara tatu na nilishinda ligi hii mara nyingizaidi  peke yangu kuliko hao makocha wengine 19 wakiunganishwa, kwa hivyo ni tatu kwangu na mbili kwao,” akasema Mourinho akinyanyua vidole vitatu hewani.

Kushindwa kwa kocha huyo katika mechi mbili kati ya tatu ilizocheza timu ya Man U si siri kunamweka katika hali ngumu Mourinho, kwani klabu hiyo haijakuwa na mwanzo mbaya kama huo tangu msimu wa 1992-93.

Vilevile, timu hiyo haijawahi kupokea kipigo cha aina hiyo ikiwa nyumbani tangu 1972, jambo linalomtia kocha huyo wasiwasi.

 

Anakaangwa kuliko Klopp na Pochettino

Lakini kile kinachoonekana kumsononesha Mourinho sasa ni kuwa licha ya rekodi yake nzuri kwenye historia ya soka, bado anazidi kukosolewa hata kuliko wenzake anaowaona kama ambao hawajafanikiwa kama yeye, ilhali wao huepuka ukosolewaji wa aina hiyo.

Msimu uliopita, Man U ilimaliza ya pili baada ya Manchester City na kabla ya msimu huo kuanza ambapo Man U ilikabiliana na Leicester kwenye mechi ya kufungua, Mourinho alikuwa ametia shauku sababu ya makocha Jurgen Klopp wa Liverpool na Mauricio Pochettino wa Tottenham kutokaangwa na wanahabari, licha ya kuwa hawakushinda kombe.

“Ni vigumu kwangu kuamini kuwa tulimaliza wa pili msimu uliopita ninapowasikiza na kusoma kwa kuwa mnaweza kufanya mtu anayemalizia nafasi ya pili kuonekana kama aliyeondolewa mapema na ambaye hakushinda kitu, mnafanya waliomaliza nyuma kukaa kama walioshinda,” akasema Mourinho.

Ni hali kama hiyo ambayo iliwahi kumfanya Bw Mourinho siku za mbeleni kumrejelea aliyekuwa meneja wa Arsenal Arsene Wenger kama ‘mtaalam katika kufeli’.

Huwa anajigamba kuwa mshindi, akisema hata akiwa United ameshinda mataji na kuingia ligi za Uropa na EFL katika msimu wake wa kwanza.

Kulingana na meneja huyo, tuzo alizoshindia Porto, Chelsea, Inter Milan na Real Madrid zinafaa kuwapa subira wakosoaji wake na zaidi wamheshimu.

Mourinho hakukosa vituko vyake vyenye kero wakati mechi dhidi ya Tottenham Hotspur ugani Old Trafford. Kando yake ni kocha mtulivu wa Spurs Mauricio Pochettino. Picha/ Hisani

 

Majigambo

Lakini majigambo yake Mourinho na kujiona shujaa hayaonekani kumsaidia, haswa wakati huu vijana wake wanapozidi kulamba chini.

Alishangaza na kufika kwake katika chumba cha kikao na wanahabari dakika 30 kabla ya muda uliopangwa Ijumaa, jambo ambalo hata Pochettino na Klopp hawajawahi kufanya, kisha kujibu kila swali aliloulizwa kwa hasira na zaidi ya yote kuondoka kabla ya kikao hicho kuisha, kwa kipindi ya chini ya dakika kumi.

Haya yote alifanya ili kuzuia wanahabari wengi kuhudhuria mahojiano yake, na kupunguza ukali wa maswali ambayo angeulizwa, hasa baada ya kuzimwa nyumbani Old Trafford na Spurs.

Ni tabia hii ya Mourinho kujiona bora kuliko kila mtu, na kujaribu kukwepa wanahabari na wakati mwingine kuwagomea kabisa kunaowachemsha waandishi wa spoti na kumchukia kwa mbinu zake chwara.

Kwa upande wao, makocha Pochettino na Klopp wamekuwa na uhusiano wa karibu sana na mashabiki wa timu zao na kupendwa na wanahabari, wakilinganishwa na Mourinho, ambaye anaishi hotelini jiji la Manchester!

Anapokuwa katika muda wake pasipo kamera, Mourinho anasemekana kuwa mcheshi, lakini kila anapotokea mbele ya vyombo vya habari, tofauti yake na Pochettino na Klopp haifichiki.

Baadhi ya wachanganuzi wamesema kuwa “The Special One” hawezi kuinoa timu moja kwa zaidi ya misimu mitatu, ukizingatia timu za Porto, Inter Milan, Real Madrid, Chelsea (mara mbili) na sasa inatazamiwa wakati wake wa kutimuliwa Man U uko karibu iwapo ataendelea kuandikisha matokeo duni.