Michezo

Soka ya Ligi Kuu ya Italia kukamilika rasmi Agosti 20

May 20th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Italia (FIGC) limeteua Agosti 20 kuwa siku ya mwisho ya kukamilika kwa Ligi Kuu ya Serie A msimu huu huku kampeni za muhula mpya wa 2020-21 ukitazamiwa kuanza rasmi mnamo Septemba 1, 2020.

Hadi kivumbi cha Serie A kiliposimamishwa kwa muda mnamo Machi 2020 kutokana na janga la corona, kila kikosi kilikuwa kimesalia mechi 12 za kusakata katika kampeni za msimu huu.

Mabingwa watetezi Juventus wanaofukuzia ufalme wa taji la Serie A kwa mara ya tisa mfululizo msimu huu, wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 63, moja zaidi kuliko Lazio ambao ni wa pili.

Kwa mujibu wa FIGC, iwapo ligi yoyote kati ya tatu za madaraja ya juu nchini Italia itasitishwa baada ya kurejelewa, basi washindi wa kila ligi na wale watakaoshushwa ngazi mwishoni mwa muhula huu wataamuliwa kwa njia ya mchujo.

Iwapo itakuwa vigumu kwa ligi hizo kukamilika kupitia mchujo, basi washindi wataamuliwa kwa matokeo yatakayokuwa yamesajiliwa na kila kikosi hadi kufikia wakati wa kusimamishwa tena kwa kampeni za muhula huu.

Ligi ya Daraja la Pili (Serie A) ndicho kitendawili kigumu zaidi kwa vinara wa FIGC hasa ikizingatiwa kwamba kipute hicho kinachojumuisha jumla ya klabu 60 tofauti ambazo zimegawanywa katika makundi matatu, kinakabiliwa na panda-shuka tele za kifedha.