Michezo

Soka ya Ligi Kuu yarejea baada ya Wizara ya Michezo kulegeza masharti ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19

November 28th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WIZARA ya Michezo imeidhinisha kurejelewa kwa mashindano ya soka, hoki na vikapu bila ya mahudhurio ya mashabiki.

Hata hivyo, michezo ya kugusana sana, ikiwemo raga, itasubiri zaidi kabla ya kuanza upya kwa hofu ya kuchangia maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

“Vikosi vya Ligi Kuu ya Soka na Team Kenya viko huru kurejelea shughuli zao. Aidha, timu za kitaifa zinazojiandaa kwa mashindano mbalimbali ya kimataifa zipo huru kuendelea kujifua. Shughuli zote nyinginezo za michezo miongoni mwa vikosi vya ligi za madaraja ya chini ni marufuku,” akasema Waziri wa Michezo, Amina Mohamed.

Mbali na soka katika kiwango cha klabu za Ligi Kuu na timu ya taifa pekee, michezo mingine ambayo imeidhinishwa kurejelewa ni voliboli, magongo, handiboli na riadha.

Kurejea kwa michezo kunatamatisha kipindi cha miezi tisa ya kusubiri baada ya serikali kupiga marufuku shughuli zote za michezo mnamo Machi kutokana na janga la corona lililovuruga sekta mbalimbali kote duniani.

Kati ya michezo ambayo itasuburi zaidi kabla ya kurejelewa kwa sababu inahusisha kugusana sana; ni raga, karate, taekwondo, uogeleaji, ndondi, scrabble na sataranji (chess).

Wizara ya Michezo imeweka michezo hii katika kategoria ya fani ambazo zina uwezo wa kuchangia maambukizi ya corona kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, mazoezi ya vikosi vya taifa katika fani hizo yataendelea chini ya kanuni kali za kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

Mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya, AFC Leopards watachuana na Tusker FC uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Novemba 28 siku ambapo Vihiga United watavaana na Kakamega Homeboyz uwanjani Mumias Sports Complex nao Bandari FC waialike Sofapaka ugani Mbaraki.

Mnamo Novemba 29, City Stars watacheza na Nzoia Sugar, Western Stima wachuane na limbukeni Bidco United nao Posta Rangers wakwaruzane na wanabenki wa KCB mjini Machakos.