Soko China: Kilimo cha avokado kunoga nchini Kenya

Soko China: Kilimo cha avokado kunoga nchini Kenya

NA SAMMY WAWERU

KILIMO cha avokado nchini kinatarajiwa kuimarika baada ya mianya ya soko la China kupanuka.

Ijumaa, makontena ya kwanza ya maparachichi mabichi kutoka Kenya yalitua nchini China, hatua ambayo imetajwa itachangia kuboreka kwa ukulima wa matunda hayo.

Mapema mwaka huu, mkataba kati ya Kenya na China mazao ya avokado kuuzwa nchini humo ulitathminiwa na kushirikisha yale mabichi yaliyokomaa.

Mnamo 2019, Kenya ilitia saini makubailiano kuuzia China maparachichi yaliyogandishwa.

Makontena manne ya avokado mbichi yaliyofika nchini humo, yalitumwa na kampuni ya Shanghai Greenchain na Sunripe Limited baada ya Beijing kuidhinisha jumla ya kampuni 15 zilizoko Kenya.

“Mwanya huo utaboresha kilimo cha maparachichi nchini. Matunda yanayoruhusishwa lazima yawe yameafikia ubora na vigezo vilivyowekwa na asasi husika,” Afisa Mkuu Mtendaji Chama cha Ushirika cha Kitaifa cha Wazalishaji wa Avokado (ASOK), Ernest Muthomi akasema.

Afisa Mkuu Mtendaji ASOK, Ernest Muthomi (kulia) na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Kilimo na Chakula anayesimamia Kitengo cha Mimea, Benjamin Tito wakielezwa kuhusu huduma za Olivado EPZ Ltd, kampuni inayosaidia wakulima wa maparachichi kupata soko nchi za ng’ambo wakati wa maonyesho ya ASOK, jijini Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Huku parachichi nchini likichezea Sh20 bei ya wastani, bei ya China inatarajiwa kuwa zaidi ya Sh120.

“Tunahitaji masoko mengi ya mazao yetu, na yanahitaji viongozi wa kisiasa walioko serikalini kujitolea kutengeneza mtandao huo,” Bw Muthomi akasema, akihimiza wakulima kuingilia ukuzaji wa avokado – wale ambao wana mashamba japo hawayalimi.

Licha ya kuwa mazao tunayopata yanakithi mahitaji ya ndani kwa ndani, afisa huyo anasema hayatoshelezi oda za masoko ng’ambo.

Mwaka 1923, Kenya ilikuwa inazalisha tani 5 za avokado na kufikia sasa imegonga tani 500, 000.

“Ni vigumu kupata maparachichi ya Kenya katika masoko ya Italia, na taswira hiyo inaashiria tuna gapu kubwa tunalopaswa kujaza,” Muthomi akasema.

Kulingana na data za Horticultural Crops Directorate, 2021 uuzaji wa maparachichi ng’ambo uliongezeka hadi kilo milioni 84.5 kutoka kilo milioni 70.3 mwaka 2020.

Ongezeko hilo aidha liliingizia Kenya mapato ya Sh15 bilioni.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO), zinaonyesha Kenya hukuza maparachichi katika hekta 230, 000, yale ya Hass na Fuerte yanayouzwa ng’ambo yakilimwa kwenye hekta 20, 000 pekee.

Wakulima wanahimizwa kukumbatia mifumo ya uongezaji maparachichi thamani.

Olivado EPZ Ltd, ni kati ya kampuni zinazotafutia wakulima soko nje ya nchi, na ina jumla ya wanazaraa 3, 000.

Shirika hilo pia huunda mafuta ya maparachichi. “Tumeanza kuongeza avokado thamani, na tumebaini bidhaa zake zina soko lenye ushindani mkuu,” asema William Magoma, afisa kutoka Olivado.

Mbali na China, masoko mengine ya avokado za Kenya ni nchi za Bara Uropa, Uingereza, milki za Kiarabu (UAE) na Urusi.

Asilimia 10 pekee ya mazao yanayozalishwa nchini ndiyo huuzwa ng’ambo.

 

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Twapongeza wanariadha wetu kuletea Kenya fahari

Raila asihi wafuasi wake wajitokeze kwa wingi wamuingize...

T L