Habari Mseto

Soko la Tononoka hatari, mtaalamu wa afya aonya

May 9th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WATAALAMU wa afya wametoa tahadhari dhidi ya sehemu hatari katika Kaunti ya Mombasa ambapo wakazi wanaendelea kukiuka maagizo ya Wizara ya Afya na kuhatarisha afya zao.

Walisema soko la Tononoka ni sehemu ambayo inaibuka kuwa hatari kufuatia idadi kubwa ya wakazi wanaokusanyika wakionya wanaeza kusambaza ugonjwa wa Covid-19.

“Nilipita soko la wazi la Tononoka nikashuhudia jinsi wakazi wanavyoendesha shughuli zao. Wanapuuza maagizo na utaratibu wa afya uliowekwa kuepuka coronavirus hivyo basi kujiweka katika hatari ya maambukizi ama kuambukizwa,” amesema Dkt Peter Sore.

Daktari huyo ameonya kwamba ukiukaji wa maagizo kama kuvaa barakoa, kusafisha mikono na hata kutokaribiana, unawaweka wakazi katika hatari ya kuambukizana Covid-19.

Alisema ugonjwa huo utaepukwa endapo wakazi watafuata kanuni zilizowekwa na serikali.

“Utasalia nasi kwa muda mrefu na kwa hivyo ni sharti tujikinge kwa kufuata kanuni dhidi ya Covid-19 kwa kuzingatia maagizo,” akasema Dkt Sore.

Katika soko hilo, Taifa Leo imewapata wafanyabiashara wakiendelea na shughuli zao bila kufuata maagizo huku wakisema uhaba wa maji ni changamoto.

Haya yanajiri huku Wizara ya Afya ikitaja kaunti za Mombasa na Nairobi miongoni mwa ngome hatari zaidi za maambukizi ya Covid-19.

Serikali ya Kaunti ya Mombasa iliwaondoa baadhi ya wachuuzi kutoka soko la Kongowea hadi Tononoka ili kukabiliana na msongamano katika soko hilo kubwa zaidi eneo la Pwani.

Hata hivyo, wachuuzi wanaomiminika Tononoka wanaendelea kujiweka katika hatari.