Habari Mseto

Soko walikofurushwa wafanyabiashara Githurai lazingirwa kwa ua

September 21st, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

HATIMAYE soko walikofurushwa wauzaji bidhaa eneo la Githurai limezingirwa kwa ua ili kuruhusu uimarishaji wa reli kuendelea.

Wafanyabiashara walioathirika wakati wa ubomoaji huo uliotekelezwa mwezi uliopita, Agosti, ni wanaouzia pembezoni mwa reli.

Shughuli za ujenzi wa ua hiyo zilianza mnamo Septemba 12.

“Wamekuwa wakichimba mashimo na kuweka vikingi vya saruji kwa zaidi ya muda wa wiki moja iliyopita,” James Kiambi, mmoja wa wafanyabiashara walioathirika ameambia Taifa Leo.

Aidha, ukuta huo unajengwa mita kadhaa kutoka kwa laini ya reli. Ujenzi huo ulianza wiki chache baada ya Gavana wa Kiambu James Nyoro kukutana na wafanyabiashara wa soko hilo ambalo ni maarufu katika uuzaji wa bidhaa za kula na mazao ya kilimo.

Bw Nyoro aliwaahidi kuwa watapata nafasi katika soko la kisasa linaloendelea kujengwa Githurai. Zaidi ya wachuuzi 1, 000 waliathirika.

Shirika la Reli Nchini limekuwa likiendeleza harakati za kufufua reli kati ya Nairobi na Nanyuki, ili kuimarisha usafiri na uchukuzi kwa njia ya garimoshi.

“Kuondolewa kwa wafanyabiashara wanaouzia kandokando mwa reli kutaruhusu kufufua uchukuzi na usafiri kwa njia ya garimoshi kati ya Nairobi na Nanyuki, na Kiambu ni miongoni mwa kaunti zitakazonufaika,” Gavana Nyoro akaambia wafanyabiashara hao alipokutana nao.

Tayari ujenzi wa vituo vya garimoshi Githurai na Ruiru, umekamilika. Ufufuaji wa reli hiyo unasemekana utasaidia kupunguza gharama ya usafiri na uchukuzi kati ya Nairobi, Thika, Karatina na Nanyuki.